*Balozi asema tatizo mawasiliano mabovu Uhamiaji
*Afuatilia
ili kumaliza mtafaruku huo kidiplomasia
Leonce Zimbandu
SIKU chache baada ya Idara ya Uhamiaji
kukamata raia wa India kwa madai ya kufanya kazi bila vibali, Balozi wa India
nchini, Sandeep Arya, ameingilia kati suala hilo na kusema tatizo lilikuwa
mawasiliano kati ya mwajiri na Uhamiaji.
Akizungumza jana na mwandishi wa gazeti
hili, Balozi Arya alisema anaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo na kudokeza
kuwa jitihada za kumaliza sintofahamu
hiyo, zinaendelea kwa njia ya mazungumzo kati ya mwajiri na Idara hiyo.
Akifafanua baada kumaliza kikao chake na
wawakilishi wa kampuni 30 za kutengeneza dawa kutoka India zinazojiandaa
kuwekeza nchini, Balozi Arya alisema baada ya kubaini tatizo kuwa mkanganyiko
wa mawasiliano, ndiyo maana wameruhusu kampuni hizo kuwekeza nchini.
“Unajua zipo ajira za muda, zingine
miaka miwili, hivyo udhaifu wa mawasiliano ulisababisha sintofahamu, hivyo
taratibu za kufanya ukaguzi zinapaswa kuchukuliwa na vibali vitolewe maisha
yaendelee,” alisema.
Balozi Arya alisisitiza kuwa jitihada za
kumaliza sintofahamu hiyo, zinaendelea kwa njia ya mazungumzo na ofisi yake kwa
kushirikiana na Serikali ya Tanzania, watahakikisha suala hilo linamalizika
kidiplomasia bila kuathiri ushirikiano uliopo.
Akizungumzia wawekezaji hao kutoka
India, Balozi Arya alisema sekta ya viwanda vya dawa India, mwaka jana iliingizia
nchi hiyo dola bilioni 16.5 za Marekani sawa na Sh trilioni 36.8 ambayo ni
asilimia 50 ya bidhaa zote zilizouzwa nje ya nchi hiyo.
Mkurugenzi wa Uhakiki wa Ubora wa Huduma
za Afya nchini kutoka Wizara ya Afya, Dk Mohamed Ally aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, alisema asilimia 80 ya dawa
zinazotumika nchini zinatoka nje ya nchi.
Alisema kati ya asilimia hizo, 60
zinanunuliwa India, hivyo ujio wa kampuni hizo ni faraja kwa Tanzania katika
kipindi ambacho nchi inatarajia kuingia kwenye uchumi wa viwanda.
“Serikali tumeandaa mazingira mazuri ya
uwekezaji, hivyo tumepata fursa ya kushawishi kampuni za dawa kujenga viwanda nchini,
ili kurahisisha upatikanaji wake kufikia malengo ya Serikali kununua dawa
viwandani,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA), Hiiti Sillo alisema wajibu wake ni kuhakikisha ubora wa
chakula na dawa nchini, hivyo lazima
usajili ufanyike kwa ajili ya ukaguzi wa ubora na kulinda usalama.
“Tuko tayari kutoa msaada kwa wawekezaji
ambao watahitaji kufahamu taratibu za usajili wa dawa na nyinginezo,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa
(MSD), Laurean Bwanakunu alihakikishia kampuni hizo za dawa kupata soko la
bidhaa zao kwa kuwa wajibu wake ni kununua dawa, kuhifadhi na kusambaza.
“Tunawakaribisha kujenga viwanda vya
dawa nchini ili kurahisisha upatikanaji wake kwani tunakabiliana na changamoto,
tunapoagiza dawa leo tunazipata baada ya miezi sita,” alisema.
0 comments:
Post a Comment