Jemah Makamba
SANAA ya uchoraji imewaponza. Ndivyo unavyoweza kusema
baada ya wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Kampala (Kiu), kilichopo Gongo la
Mboto Dar es Salaam, kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini humo,
kwa tuhuma za kuchora na kusambaza picha zinazomdhalilisha Rais John Magufuli.
Wanafunzi hao Amenitha Harod (19), Mariam Tweve (20),
Agnes Sutta (21) na Anne Mwansasu (23), walisomewa mashitaka hayo na Mwendesha
Mashitaka wa Serikali, Florida Wenceslaus, huku wakikana tuhuma hizo na
kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Catheline Kiyoja,
Wenceslaus alidai washitakiwa walitenda kosa kinyume na Kifungu cha Sheria cha
16 cha Makosa ya Mtandao sura ya 14 kama kilivyorekebishwa mwaka 2015.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba washitakiwa wote kwa
pamoja wakiwa jijini Dar es Salaam Juni 9 mwaka jana, walisambaza picha ya
kuchora kwa nia ya kumtukana na kumdhalilisha Rais Magufuli.
Wenceslaus aliendelea kudai washitakiwa hao wote kwa
pamoja walichora picha inayomuonesha Rais amevaa kitu kama hijabu,
wakimfananisha na mwanamke kwa nia ovu, huku wakijua ni kosa kisheria.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo washitakiwa walipoulizwa
na Hakimu kama wametenda kosa hilo, wote walijibu si kweli.
Mwendesha mashitaka aliileza Mahakama kuwa upelelezi wa
kesi hiyo bado haujakamilika, lakini dhamana za washitakiwa ziko wazi kama watakidhi
masharti watakayopewa.
Masharti ya dhamana waliyopewa ilikuwa ni wadhamini
wawili wa kuaminika wanaofanya kazi katika taasisi za Serikali au sekta
zinazotambulika, wasaini ahadi ya maneno ya Sh milioni 2 kwa kila mmoja.
Washitakiwa wote walishindwa kukidhi masharti ya dhamana na
kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 13 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment