Vigogo 6 wa Ushirika mbaroni


Julius Konala, Songea

VIONGOZI sita na watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika vya wilaya za Songea na Namtumbo, wamekamatwa na Polisi mkoani Ruvuma kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha na mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Sonamcu.

Akizungumza jana mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani ambaye pia ni Mbunge wa Namtumbo, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya uchunguzi wa tume ya maendeleo ya ushirika kutoka makao makuu Dodoma.

Watuhumiwa hao ambao baadhi yao wako mikononi mwa Polisi ni Ally Bango, Edwin Ngonyani, Eletius Ngonyani, Awadhi Nyoni, Habibu Likonda na Eva Kihwili ambao watafikishwa kwenye vyombo vya kisheria kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mgema alisema vitendo vya ubadhirifu wa baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama hivyo kwa kushirikiana na viongozi wa chama kikuu cha ushirika cha wilaya ya Songea na Namtumbo, vimechangia kukatisha tamaa wakulima wa tumbaku.
Alisema vitendo hivyo vimeendelea kuwadidimiza kwenye dimbwi la umaskini hali ambayo haipaswi kuendelea kufumbiwa macho huku wahusika wakiendelea kuwapo.

Mgema alisema baadhi ya watumiwa wa ubadhirifu huo ni viongozi na watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika na chama kikuu cha ushirika ambao walipewa dhamana ya kuongoza wanachama wa ushirika huo.
Badala ya kuongoza wanachama, Mgema alisema viongozi hao walikwenda kinyume na tafsiri halisi ya ushirika, kwani baadhi yao walitumia vibaya dhamana walizopewa hivyo kustahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sharia, ili kuwa fundisho kwao na wengine.

Akitaja jinsi ubadhirifu huo ulivyofanywa, msimamizi na mdhibiti wa vyama vya ushirika wa tume hiyo, Gabinus Mtonga alisema viongozi hao kwa nyakati tofauti waliendesha chama hicho bila kufuata taratibu za ushirika, wakipokea na kutumia fedha bila taratibu na sheria za ushirika licha ya kupewa maelekezo ya mara kwa mara na wakaguzi wa mahesabu wa ndani na nje na ushauri kutoka kwa Mrajisi msaidizi wa ushirika wa mkoa.

Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu wa Tume makao makuu, Kawina Kawina akihitimisha taarifa za tuhuma za ubadhirifu huo wa zaidi ya Sh bilioni moja na kutaja watuhumiwa sita, alisema ubadhirifu huo haupaswi kushughulikiwa kwa sheria za ushirika pekee bali za nchi pia zinahusika, kwa sababu baadhi ya vitendo vilivyofanywa vinaingia kwenye makosa ya jinai.
  
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo