Hussein Ndubikile
WAENDESHA bodaboda wa Dar es Salaam,
wamesisitizwa kutekeleza agizo la Rais John Magufuli linalopiga marufuku
bodaboda na bajaji kupita kwenye barabara ya mabasi yaendayo haraka (Udart) ili
kuepuka usumbufu wa kupelekwa mahabusu na kutolewa matairi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Jeshi la
Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, kuanza kutekeleza agizo hilo kwa
kukamata pikipiki 21 na kuzitoa matairi kisha kuwapeleka mahabusu madereva hao.
Akizungumza na gazeti hili jana, ofisa
habari wa waendesha bodaboda hao, Abdallah Bakari alisema madereva hao
wanapaswa kujua barabaara yanamopita mabasi ya mwendokasi hivyo hakitakiwi
chombo kingine na kwamba dereva atakayekaidi atakumbwa na adhabu hiyo.
“Barabara ya mwendokasi inatumiwa na
mabasi yake tu yanayoanzia Kimara hadi Feri, haitakiwiki bodaboda unashauriwa
ukitaka kuvuka upande wa pili wa barabara ya mabasi hayo, tafuta sehemu yenye
kivuko, shuka, sukuma pikipiki mpaka upande wa pili usipite eneo wanalopita waenda
kwa miguu,” alisema.
Alisema bodaboda haitakiwi kuvuka eneo lisilo
na alama ya kivuko huku akiwasihi kuacha kufanya biashara Feri na barabara ya
Morogoro kwani kufanya hivyo ni kukaidi sheria za barabarani.
Alisisitiza kuwa kikosi hicho
kimejipanga maeneo yote ambayo barabara hiyo imepita na atatoa ushirikiano
kuhakikisha agizo la Rais Magufuli linatekelezwa.
Hivi karibuni, katika uzinduzi wa mradi
huo, Rais Magufuli aliagiza kikosi hicho kukamata waendesha bodaboda na bajaj
wanaokatisha kwenye barabara ya mwendokasi na kuwatolea matairi.
0 comments:
Post a Comment