*Kamishina asema baadhi wamekuwa wakikwamisha vita
*Wengine wajifanya madaktari ili kutetea
watuhumiwa
Suleiman Msuya na Hussein Ndubikile
Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma |
SASA ni dhahiri kwamba vita dhidi ya
mihadarati itatikisa pia majaji na mahakimu nchini baada ya jana Kamishna wa
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga kutangaza kuandaa
orodha ya wanaokwamisha vita hivyo, ili wachukuliwe hatua stahiki.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye
mkutano ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Makonda, Sianga alisema wapo majaji
na mahakimu ambao wamekuwa wakiharibu kesi za dawa za kulevya kwa makusudi.
Katika mkutano huo ambao alikabidhiwa
majina 97 ya vigogo wa dawa za kulevya na Makonda, Sianga alisema katika
kuendeleza vita hivyo wameandaa ripoti ya majaji, mahakimu, watumishi wote
ambao wamekuwa wakiharibu kesi zinazofikishwa mahakamani.
Kamishina huyo alisema ushahidi unaonesha
kuwepo tabia ya baadhi ya majaji na mahakimu kuharibu ushahidi jambo ambalo
linakwamisha jitihada za Serikali kupambana na dawa za kulevya nchini.
“Katika kuonesha kuwa tuko tayari
kukabiliana na tatizo hili, tunataka kuanza na majaji na mahakimu ambao kwa makusudi
wamekuwa wakivuruga na kuharibu kesi za dawa za kulevya, tunaanza nao, ila wapo
watumishi ambao wameidhinisha viuatilifu ambavyo haviruhusiwi tutashughulika
nao,” alisema.
Kamishina Sianga alisema hakuna mtu aliye
juu ya sharia, hivyo dhana ya usawa katika mihilimi ya Dola ikiwamo Bunge na
Mahakama, lazima izingatiwe bila kuangalia mtu fulani.
Alitolea mfano kesi ya Tanga ambako
mtuhumiwa aliingiza kilo 50 na jaji kutoa uamuzi kuwa hakuna ushahidi ni lazima
taarifa ziende kwa Jaji Mkuu.
Aidha, alisema yuko mtu alikutwa na kete
180 tumboni, lakini uamuzi wa jaji katika kesi hiyo ukasema mhusika alikuwa na
vidonda vya tumbo, hali ambayo inakwamisha jitihada za Mamlaka.
Aliongeza kuwa kuna mikoa ambayo majaji
na mahakimu walijivisha majukumu ya udaktari kwa kutetea washitakiwa waziwazi
kuwa hawajihusishi na biashara ya mihadarati hiyo wakati walikamatwa na
vidhibiti.
Alifafanua kuwa wafanyabiashara wa dawa
hizo wakiachwa wataliletea Taifa madhara makubwa, ikiwamo kuchangia ugumu wa
maisha na kuharibu nguvukazi ya Taifa.
Pia alisema matumizi ya dawa za kulevya
yanasababisha madhara mengi katika jamii yakiwamo ya kiakili, kiafya na
kiuchumi.
Aidha, alisema wanatafuta watumishi walioingiza
viuatilifu tani 21 ambavyo vinatumika kuchanganywa na dawa za kulevya huku
wakijua ni kosa kisheria.
Alisema hakuna ofisa aliyehusika
atakayeachwa na hawataangaliwa vyeo badala yake watafikishwa kwenye vyombo vya
sheria na kuchukuliwa hatua kama watu wengine.
“Kuna walioshiriki kuingiza viutalifu
kinyume na sheria hawataachwa, wote waliohusika watakamatwa na kuchukuliwa
hatua kama watu wa kawaida na Kamishna Mihayo Msikhela ameanza kazi hiyo,”
alisema.
Alisema kila mtu anapaswa kutimiza
majukumu kwa mujibu wa sheria na endapo atakwenda kinyume, amejipanga
kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kukabiliana na hali hiyo.
Aidha, alisema atahakikisha makundi
ambayo yameathirika yanapata tiba na huduma ya elimu ya kuelewa madhara kama
njia ya kukabiliana kwa hatua ya awali.
Sianga alisema kipaumbele chake ni
kukabiliana na biashara ya bangi na mirungi ambayo inapatikana nchini kabla ya
kuongeza nguvu katika dawa zinazotoka nje.
Alisema madhara ya mirungi ni kupata saratani
na kupunguza nguvu za kiume huku bangi ikisababisha mtu kuwa na maruweruwe.
Sianga alisema takwimu za mwaka jana
zinaonesha tani 20 ziliingia katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, hali
ambayo inaonesha tatizo ni kubwa.
Akizungumza kwenye kipindi cha Mizani ya
Wiki, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Dawa za Kulevya, Dk Faustine
Ndungulile alisema takwimu zinaonesha zaidi ya Watanzania 250,000 wanatumia
dawa za kulevya.
0 comments:
Post a Comment