Mwandishi Wetu, Kiteto
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
hiyo, Tamim Kambona kwenda kata ya Engusero keshokutwa kufanya mkutano wa
hadhara na kujibu kero za wananchi wa kata hiyo.
Viongozi hao wametakiwa pia wafuatane na
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Lairumbe Mollel wakatoe ufafanuzi bila kukosa.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana kijijini
Engusero wilayani hapa baada ya kusimamishwa na wananchi akiwa njiani kwenda Kibaya
yaliko makao makuu ya wilaya hii kuanza ziara ya kikazi mkoani Manyara.
Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na
wananchi wa Engusero, Waziri Mkuu alichukua ombi la wakazi hao la kujengewa
soko la kimataifa ili wauze mahindi yao hapo hapo.
“Nitaawagiza Mkuu wa Wilaya na
Mkurugenzi wa Halmashauri waje hapa Jumamosi hii na kufanya mkutano ili wawaeleze
wana mpango gani kuhusu soko hilo,” alisema.
Awali, mkazi wa kata hiyo, Ali Athumani
alimwomba Waziri Mkuu awasaidie ili kujengewa soko la kimataifa kwa sababu wao
ni wazalishaji wakubwa wa mahindi, lakini hawafaidiki nayo kwa sababu yote yanauzwa
soko la Kibaigwa.
Said Shabani alimwomba Waziri Mkuu
awasaidie kufuatilia upatikanaji gari la wagonjwa na ujenzi wa wodi nyingine ya
na mochari kwenye zahanati yao.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema
Serikali imeweka nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya na kuwataka
watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji wadhibiti kadhia hiyo.
“Tunataka vijiji vyetu, kata zetu,
wilaya zetu na mikoa yetu iwe safi bila hata chembe ya dawa za kulevya.
Tukikuona kijana unayumbayumba au kuweweseka, tunakupima na tukikuta umetumia
ile kitu, tunakukamata ili utwambie nani amekupa,” alisema na kuongeza:
“Sisi tunataka vijana wafanye kazi za
kujiletea maendeleo. Kijana hawezi kuwa na maendeleo wakati hafanyi kazi, hawezi
kuwa na ndoto za maendeleo wakati amelewa bangi au dawa za kulevya. Kila mmoja
afanye kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment