Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu,
Kassim Majaliwa, ametaka mabalozi wa Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani, kuhakikisha
wanatumia uwakilishi wao kutafuta wawekezaji kwenye sekta ya viwanda nchini.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuimarisha uchumi hadi wa
kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu la mabalozi hao ni kuhakikisha
jambo hilo linafanikiwa.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana, alipokutana na
mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China,
Italia, Ufaransa, DR Congo na Uswisi.
Mabalozi hao ni Dk Emmanuel Nchimbi (Brazil), Elizabeth
Kiondo (Uturuki), George Madafa (Italia), James Msekela (Uswisi), Samuel
Shelukindo (Ufaransa), Paul Mella (DRC), na Mbelwa Kairuki (China).
“Serikali inahitaji watu wa kuja kuwekeza katika viwanda
ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza nje ya nchi, hivyo jukumu lenu
ni kuhakikisha tunapata wawekezaji wenye sifa,” amesema.
Pia Waziri Mkuu aliwataka mabalozi hao kutumia uwakilishi
wao kwenye nchi hizo kwa kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii nchini ili
kuongeza idadi ya watalii wanaokuja.
“Tulinde bidhaa za ndani ya nchi yetu, mfano madini ya
tanzanite ambayo yanazalishwa Tanzania pekee, lakini leo yanasababisha nchi zingine
kusifiwa kwa uzalishaji zikiwamo India na China, hivyo jukumu lenu ni
kuhakikisha mnatangaza madini yetu ipasavyo,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka mabalozi hao kulinda
maslahi ya Taifa kwenye nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano kati
ya Tanzania na mataifa hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka
mabalozi hao kuwatambua Watanzania wanaoishi kwenye mataifa hayo na
kushirikiana nao kutafuta wawekezaji kuwekeza nchini.
Balozi Mella ambaye alizungumza kwa niaba ya mabalozi
wenzake, alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba watatekeleza wajibu wao ipasavyo.
0 comments:
Post a Comment