Wapinzani wamsusia tena Dk Tulia


Fidelis Butahe, Dodoma

WABUNGE wa Upinzani jana kwa mara nyingine, walitoka ndani ya ukumbi wa Bunge wakipinga kauli ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuhusu Polisi kukamata wabunge wa kambi hiyo.

Hatua hiyio ilianzia kwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) baada ya kuwasilisha hoja bungeni akipinga wabunge kukamatwa na Polisi kwa alichoeleza kuwa hakuna sababu za msingi.

Lakini pia akabainisha kuwa hata yeye alipewa taarifa kuwa akitoka nje ya eneo la Bunge atakamtwa na Polisi kwa tuhuma asizozijua.

Zitto alitoa kauli hiyo jana saa 10.35 jioni mbele ya waandishi wa habari baada ya wabunge wa Upinzani kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge kutokana na kueleza kutoridhishwa na kauli ya Naibu Spika, kupinga hoja hiyo.

Awali, Dk Tulia alilaimbia Bunge jinsi alivyopata ujumbe wa maandishi kutoka kwa Zitto ukimwomba ampe nafasi ya kutoa taarifa kuhusu suala alilokuwanalo baada ya kumkatalia kufanya hivyo asubuhi.

Baada ya kauli hiyo, Zitto alisimama na kuliambia Bunge, kwamba utaratibu wa Polisi kukamata wabunge wa Upinzani unakiuka Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.

“Bunge letu liko nchi za Jumuiya ya Madola na linaongozwa na Katiba, kanuni, sheria za mabunge mengine, uamuzi wa maspika wengine na sheria zingine,” alisema.

“Hivi karibuni, Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema), alikamatwa nje ya Bunge baada ya kuhudhuria vikao vya Bunge na hadi sasa Bunge halina taarifa.”

Alisema kwa mujibu wa nchi za Jumuiya ya Madola, polisi wanapotaka kukamata mbunge, lazima wampe taarifa Spika naye Spika aliambie Bunge juu ya taarifa hiyo na kueleza ni kwa nini mbunge anakamatwa.

Alisema hata Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali amefungwa miezi sita jela bila Bunge kuelezwa chochote juu ya tukio hilo, jambo ambalo ni kinyume na sheria hiyo, huku pia akigusia kukamatwa kwa Tundu Lissu (Singida Mashariki).

Lissu alikamatwa juzi saa 12 jioni wakati akielekea lango la kutoka bungeni na kusafirishwa usiku kwenda Dar es Salaam kwa tuhuma ambazo hazikuwekwa wazi.

“Hata mimi nimepata taarifa, kwamba polisi wananisubiri ili nikitoka nje wanikamate na siogopi kukamatwa. Naomba jambo hili lijadiliwe na kulitolea uamuzi,” alisema na kumtaja mbunge wa Nzega Mjini, Dk Hamisi Kigwangalla (CCM) kuwa naye aliwahi kukamatwa kwa mtindo huo.

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Dk Tulia alisema sheria ziko hivyo, Bunge haliwezi kufuata sheria za mabunge mengine na kwamba jambo hilo halihusu makosa ya madai, hivyo haliwezi kujadiliwa.

Baada ya majibu hayo, wabunge walionekana kutoridhishwa, huku wakiwa wamesimama walipingana na uamuzi huo jambo lililomlazimu Dk Tulia kumtaka Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha (chadema) atoke ukumbini.

Mbunge huyo aligoma, jambo lililomlazimu Naibu Spika kuita askari wa Bunge kumtoa Chacha na kusababisha wabunge wote wa Upinzani kusimama na kutoka huku wakitoa maneno ya kumponda Dk Tulia ambaye aliwataka watoke kwa utaratibu bila vurugu.

Nje
Zitto akiwa na wabunge wengine wa Upinzani alisema kutokana na taarifa kuwa anasakwa na Polisi, hatatoka nje ya eneo la Bunge.

“Sitoki nje kabisa hivi sasa nakwenda maktaba kujisomea,” alisisitiza.

Mdee
Mapema Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee alihoji sababu za Lissu kukamatwa.

Wakati Mbunge huyo akitaka kujua sababu jana, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilizitaja likisema lilifanya hivyo ili kumhoji huku Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro akisema Lissu alikamatwa kwa amri yake kutokana na kauli alizotoa zikiashiria uvunjifu wa amani.

Mwanasheria Mkuu huyo wa Chadema juzi alihudhuria kikao cha sita cha Bunge na mara baada ya kukamatwa, dereva wake, Simon Makira aliiambia JAMBO LEO kuwa Lissu alipowahoji polisi sababu za kumkamata, walimjibu ni kutokana na kauli zake juu ya upungufu wa chakula katika baadhi ya wilaya nchini.

“Jana (juzi) Lissu alikamatwa na polisi katika eneo la Bunge karibu na lango na kusafirishwa usiku kwenda Dar es Salaam. Nimeliuliza hili maana kilichotokea kwa Lissu ndicho kilichotokea kwa Lema (Godbless-Mbunge wa Arusha Mjini) miezi kadhaa iliyopita, ambaye yuko ndani wakati kosa lake ni dogo la kupewa dhamana,” alisema Mdee

“Naomba Mwongozo wako, unadhani ni sahihi vitendo vinavyofanywa na polisi ambao sijui wanapewa kiburi na nani kudhalilisha wabunge wakiwa kwenye majukumu yao ya kawaida ya kibunge?” Alihoji Mdee.

Akijibu Mwongozo huo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alisema jambo hilo hawezi kulitolea Mwongozo, kwa kuwa halikutokea ndani ya chombo hicho.

Sababu za kukamatwa kwa Lissu kwa mujibu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ni matamko aliyowahi kuyatoa kipindi cha nyuma ambayo ni ya uchochezi.

“Siwezi kutaja matamko ambayo yamesababisha tumkamate nitataja wakati mwingine, lakini ifahamike tu kwamba matamko yake ya nyuma yaliashiria uvunjifu wa amani, hivyo akimaliza kuhojiwa tutaweka wazi hatua zinazofuata,’’ alisema Sirro na kuongeza:

“Ikiwa atapelekwa mahakamani nitaweka wazi na kama ataachwa pia tutasema, kwa sasa hatuwezi kuingilia mahojiano yanayoendelea.”

Alisema Lissu alitoa maneno ya uchochezi ambayo haikuwa lazima kukamatwa kwa wakati huo kabla uchunguzi haujakamilika.

Alipoelezwa kuwa Jeshi hilo lilimwita Lissu mwishoni mwa mwaka jana na kumhoji kuhusu maneno aliyotoa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kupotea kwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane, lakini likamwacha, alisema si kosa kumwacha na kumkamata tena.

“Ni kweli tulimwita Lissu alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu na kupotea kwa Saanane, ambapo alitoa kauli nyingi ikiwamo kuhusisha Polisi na kutesa wananchi katika nyumba aliyodai kwamba ipo Mikocheni, lakini tulimwacha sasa tumeamua kumwita tena na si kosa kufanya hivyo,’’ alisema.

Kamanda Sirro aliongeza: “Sheria haikatazi mtu uliyemhoji leo (jana) ukamruhusu akawa huru, usimkamate tena baada ya kufanya uchunguzi wako, mtu anaweza kukaa uraiani hata miaka miwili baada ya kuhojiwa, lakini baadaye akaja kukamatwa tena na kutiwa hatiani, inategemea uchunguzi ulifikia wapi wakati huo.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo