Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,
imeshindwa kutoa hukumu ya kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Kampuni ya Jamii
Media ambayo ni wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya Jamii Forums na
FikraPevu kwa sababu jalada la kesi hiyo halijulikani lilipo.
Wakili wa Kampuni hiyo, Bernedict Alex alisema jana nje
ya mahakama hiyo kuwa kutokana na rekodi za mahakama faili hiyo halikuonekana
hivyo imeshindwa kutoa hukumu.
Alisema walikwenda kwa karani ambaye ndiye anayehusika na
kesi hiyo na kulitafuta jalada la kesi hiyo bila mafanikio, wakaendelea kufuatilia
na kubaini kuwa mmoja wa jopo la majaji wa tatu, Jaji Winfrida Koroso
amehamishiwa katika Mahakama ya Kifisadi.
“Tumekubaliana na mawakili wa Serikali kulifuatilia suala
hili ili tujue mwafaka wa kesi yetu,”alisema Wakili Alex. Kesi hiyo ilikuwa
inasikilizwa na Koroso, Jaji Isaya Arufani na Jaji Ignus Kitusi.
Jamii Media waliamua kufungua kesi hiyo kutaka kifungu cha
32 na 38 cha sheria ya Makosa ya Mtandao viangaliwe upya kwani vinasababisha
kuvunjwa kwa haki za msingi za Watanzania watumiao mitandao.
Pia, walifungua kupinga amri waliyopewa na polisi ya
kutoa taarifa binafsi za wanachama wao dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG) na Jeshi la Polisi Awali, Wakili wa Jamii Media, Shukuru Mkwafu alisema
ili kulinda masilahi ya umma, lazima vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vizingatiwe.
Alisema Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015,
inakiuka haki ya kikatiba namba 16 inayoruhusu kuwapo na hali ya faragha na
kifungu namba 18 kinazungumzia uhuru wa kujieleza.
Mkwafu alisema baadhi ya vifungu vya sheria ya kimtandao
vinakiuka masharti ambayo yamewekwa na katiba hasahasa vinaingilia haki ya faragha
ambayo wateja wetu wanayo kikatiba, kwa hiyo wanaiomba mahakama ibatilishe na itamke
kuwa vifungu hivyo ni batili kwa kuwa vinaenda kinyume na ibara 16 na 18 ya
katiba.
Hatua hiyo ya kufungua shauri Mahakamani imekuja baada ya
kuwepo na shinikizo kutoka Jeshi la polisi kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii
Maxence Melo kutoa taarifa za baadhi ya wateja wake.
0 comments:
Post a Comment