Fidelis Butahe na Abraham Ntambara
Freeman Mbowe |
HATIMAYE Jeshi la Polisi jijini Dar es
Salaam jana limefanikiwa kumkamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
kumhoji kwa saa kadhaa kabla ya kuondoka naye ikielezwa kuwa amekwenda
kupekuliwa nyumbani kwake.
Mbowe amekuwa akisakwa na jeshi hilo kwa
takriban siku 10 tangu alipotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda alipotaja majina ya watu 65 waliodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo
zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Chama hicho zinaeleza kuwa Mbowe alikamatwa eneo la Kawe jijini
humo.
Februari 10 mwaka huu, Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema Mbowe anatakiwa kuripoti
kituo kikuu cha Polisi na kwamba asipofanya hivyo bila kutoa taarifa yoyote ya
hudhuru, atasakwa popote alipo.
Sirro alitoa kauli hiyo saa chache baada
ya Mbowe kuzungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kubainisha kuwa hatakwenda
kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam hadi atakapopewa
wito maalum wa kisheria unaomtaka afike kituoni hapo.
Mbowe ni miongoni watu 65 waliotajwa na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kutakiwa kuripoti kituo kikuu
cha polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu biashara na autumiaji wa dawa za
kulevya.
Utaratibu huo tata wa kutaja majina
ilikuwa ni awamu ya pili baada ya ule ya kwanza kuwalenga wasanii zaidi,
Waliotajwa katika awamu hiyo ya pili ni
wafanyabiashara wadogo na wakubwa, viongozi wa dini na wamiliki wa hoteli na
migahawa, huku Makonda akieleza kuwa wanaweza kuwa na taarifa zitakazosaidia
polisi kuwabaini wauzaji wa dawa hizo.
“Alikuwa akitoka nyumbani kwake kuelekea
polisi kuitikia wito wao, lakini alipofika eneo la Kawe alimkamata na kumpeleka
kituoni,” alisema Makene.
“Mpaka sasa (jana jioni) hatujui
amekamatwa kwa kosa lipi na nini ambacho kinaendelea isipokuwa tu katika
mahojiano hayo yupo pamoja na wakili.”
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho
Zanzibar, Salum Mwalimu naye alisema Mbowe alikamatwa saa tisa alasiri,
kubainisha kuwa anahojiwa na kikosi kazi maalumu cha Jeshi la Polisi.
“Mimi nikiambatana na Wakili wa chama,
Frederick Kihwelo tumefika kituoni hapa muda mfupi baada ya Mbowe kufika, lakini
tumezuiwa kumuona, tukielezwa tutaruhusiwa kufanya hivyo atakapomaliza
mahojiano au hatua ya kurekodi mahojiano,” alisema Mwalimu.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Waziri Mkuu
wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amekatisha mapumziko
yake kijijini kwake Monduli kufuatilia kukamatwa kwa Mbowe na anatarajiwa
kuwasili jijini humo leo.
Gazeti hili lilipomtafuta Sirro kwa njia
ya simu, ilipokelewa na msaidizi wake na kubainisha kuwa Kamanda huyo alikuwa
katika mkutano.
Habari zaidi zinaeleza kuwa jana saa 11
jioni, ulinzi uliimarishwa katika kituo kikuu hicho cha polisi na baada ya nusu
saa Mbowe aliondolewa eneo hilo na polisi kwa kutumia gari namba T 886 BMX aina
ya Land Cruiser.
Licha ya polisi kutotoa maelezo yoyote
mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, taarifa zaidi zinaeleza kuwa mbunge
huyo wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni alikuwa akipelekwa
nyumbani kwake kupekuliwa.
Siku chache baada ya Mbowe kutajwa
katika orodha hiyo, Chadema kilifungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu dhidi ya
Makonda kwa kukiuka sheria na taratibu katika kushughulikia watuhumiwa wa
biashara ya dawa za kulevya.
Katika mkutano wake na wanahabari mjini
Dodoma Mbowe alipinga vikali kujihusisha na biashara hiyo akiwa sambamba na
wabunge wa upinzani.
“Nina mambo matatu ya kuzungumza;
kwanza, ninakanusha kwa nguvu zote kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya
kwa sababu katika maisha yangu, sijawahi kujihusisha na biashara hiyo au hata
kutumia dawa za kulevya,” alisema Mbowe katika mkutano huo
“Pili, sisi kama wapinzani,
tunakubaliana na mapambano dhidi ya dawa hizo kwa sababu ni hatari katika
maisha yetu na tunaona vita hii ilitakiwa ipiganwe miaka mingi iliyopita,
lakini kutokana na sababu mbalimbali, haikupiganwa.”
Jambo la tatu, Mbowe alisema Makonda
siyo polisi na kwa mujibu wa sheria, hana mamlaka ya kuita mtu polisi ingawa
yeye ni kiongozi wa mkoa.
0 comments:
Post a Comment