Suleiman Msuya
Ukumbi wa Nkrumah |
WAHADHIRI wametaja zaidi ya sababu 10
zinazochangia vyuo vikuu nchini kukosa sifa za kuingia kwenye ubora wa vyuo
Afrika Mashariki, Afrika na Duniani, huku kutofanya utafiti kukitajwa kama
sababu kuu.
Sababu hizo zimetajwa siku chache baada
ya Taasisi ya Webometrics ambayo inajihusisha na kupanga ubora wa vyuo vikuu kutaja
vyuo bora 100 Afrika huku Tanzania ikiingiza vyuo vitatu kwenye 10 bora.
Akizungumza na JAMBOLEO jana, Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa,
alizitaja sababu hizo kuwa ni ukosefu wa utafiti, idadi ya wanafunzi, walimu
wenye Shahada ya Uzamivu na maprofesa, kutobadilishana wahadhiri na wanafunzi kutoka
nje.
Dk Mkonongwa alisema sababu nyingine ni
sifa za wanafunzi wanaodahiliwa na programu ambazo zinafundishwa kuwa za
kimataifa.
“Chuo kikuu ni taasisi za kimataifa,
hivyo ili uweze kuingia kwenye ushindani, mambo mengi huangaliwa hasa utafiti,
jambo ambalo kwa wahadhiri wa Tanzania halifanyiki kutokana na kutumia muda
mwingi kufundisha na kusahihisha mitihani,” alisema.
Mhadhiri huyo alisema wahadhiri wengi wa
Tanzania wanafundisha zaidi ya wanafunzi 2,000 jambo ambalo linasababisha
washindwe kutumia muda mwingi kufanya kazi za kijamii.
Alisema wakati Tanzania ikikabiliwa na
mazingira hayo, katika vyuo vilivyondelea hali ni tofauti ambapo mwalimu
anaweza kufundisha wanafunzi wasiozidi 200, hivyo kutumia muda mwingi kuandika
machapisho ya kitafiti.
Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere
(MNMA), Dk Thomas Ndaluko alisema pamoja na changamoto zingine, anaamini
miundombinu, machapisho kidogo na mafunzo adimu kwa walimu ni sababu mojawapo.
Dk Ndaluko alisema ili kuingia kwenye
ubora wa kidunia na Afrika, ni kazi ambayo inachukua muda mrefu hasa katika
nchi ambazo hazijawekeza kwenye elimu ipasavyo.
“Si jambo la siku moja, ndiyo maana sisi
hapa MNMA tumeamua kuruhusu walimu takribani 50 waende kusoma uzamivu, ili kuwa
na watu sahihi katika sekta hiyo,” alisema.
Alisema kwa sasa wana mkakati wa
kubadilishana wahadhiri na vyuo vitatu vya nje, huku wakijiandaa kupokea
wanafunzi kutoka nje.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU),
Lusekelo Kwasongwa alisema vigezo vinavyutumiwa ni vingi, huku akibainisha
kigezo kimojawapo kuwa ni maktaba za kutosha na walimu bora kitaaluma.
Kasongwa alisema vyuo vingi nchini vina
uhaba wa walimu hasa wenye sifa ya uzamivu, hivyo ni vigumu kuingia kwenye
ushindani wa taasisi hiyo.
Alisema pia vyuo vingi havijihusishi na utafiti
hiyo ikichangiwa na changamoto za kifedha hivyo kuwa vigumu kuwa miongoni mwa vyuo bora Afrika au Afrika Mashariki.
Katika ripoti hiyo, Chuo Kikuu cha
Rwanda kilikuwa kikiongoza kwa ubora siku hadi siku ambapo kati vyuo 26,300 Afrika
ikiwa na vyuo 1,520 chuo hicho kilifanikiwa kuwa katika 100 bora kwa kushika
nafasi ya 96 kutoka 123 Julai mwaka jana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Chuo hicho
mwaka huu kimeshika nafasi ya 3,499 kutoka ya 3,907.
“Chuo hiki kimefanya vizuri kwani
kimeingia 10 Bora ya EA kutoka nafasi ya 11 mwaka jana ila pia katika ukanda wa
Kusini mwa Jangwa la Sahara kiko nafasi ya 52 kutoka 67 ya mwaka jana,” ilisema
taarifa.
Ripoti hiyo ilisema Januari mwaka jana,
chuo hicho kilikuwa cha 140 Afrika na 72 Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hali kadhalika taarifa hiyo inaonesha kuwa
katika Afrika Mashariki Chuo Kikuu cha Nairobi, ndicho kinaongoza kikishika
nafasi ya nane Afrika kikifuatiwa na Makerere cha Uganda ambacho kwa Afrika ni
cha 11.
Vingine kwenye 10 bora ni Kenyatta, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jomo Kenyatta, cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na cha
Teknolojia cha Jomo Kenyatta, Mbarara cha Uganda, Chuo Kikuu cha Afya, Sayansi
ya Tiba Muhimbili (MIHAS) na Egerton cha Kenya.
0 comments:
Post a Comment