Hussein Ndubikile
UMOJA wa Wainjilisti wa Kikristo
Tanzania (Uwakita) umeipongeza Serikali kwa kazi nzuri inazoendelea kufanya, ikiwemo
kusimamia nidhamu ya kazi, kutetea wanyonge, kukusanya kodi, kupambana na
ufisadi na kuhamasisha usafi wa mazingira.
Mjumbe wa umoja huo, Elieza Shinza
alisema tangu Rais John Magufuli achaguliwe kuiongoza nchi, amekuwa mstari wa
mbele kusimamia nidhamu ya watumishi wa umma na uwajibikaji.
“Tunapenda kumpongeza Rais Magufuli na
Serikali yake kwa kazi anazozifanya. Anatetea wanyonge, anasimamia ukusanyaji
kodi na kupambana na ufisadi,” alisema.
Alisema rais Magufuli ni kiongozi wa
kuigwa kutokana na msimamo alionao wa kuwapigania watu wa hali ya chini na
kuvikataa vitendo vya rushwa ndani ya Serikali.
Katika hatua nyingine, umoja huo umeomba
kupatiwa ufafanuzi kuhusu ziara ya mfalme, Mohamed VI wa Morocco iliyofanyika
nchini mwishoni mwa mwaka jana ilikuwa ni ya Kiserikali au ya kidini.
Shinza alisema ombi la ufafanuzi huo
limetokana na kwamba kiongozi huyo anatambulika kama kiongozi wa Kiserikali na
kiongozi mkuu wa dini katika nchi yake, hivyo ni vyema suala hilo
likafafanuliwa kuondoa utata uliojengeka.
Alisema licha ya kusainiwa mikataba ya
kimaendeleo baina ya nchi hizo, huku akiongeza rais Magufuli aliutangazia umma
kuwa amemwomba mfalme huyo kumjengea msikiti jijini Dar es Salaam na kwamba
ilikuwa halali kwa rais kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa Uwakita unaomba kufahamu
kuwa rais kuomba kujengewa msikiti ni kipaumbele cha nchi.
0 comments:
Post a Comment