Fidelis Butahe, Dodoma
Freeman Mbowe |
MWENYEKITI
wa Chadema, Freeman Mbowe, ameunda kamati ya watu watano kusaka mwafaka wa
matumizi ya Sh bilioni 5.8 za uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafiri Dar es
Salaam (Uda) sambamba na mkakati wa kudumu wa kumaliza tatizo la usafiri Dar es
Salaam.
Kamati
hiyo iliundwa baada ya kumalizika kwa kikao kati yake na mameya, naibu mameya wa
Jiji hilo pamoja na viongozi waandamizi wa vyama vinavyounda Ukawa,
kilichofanyika kwenye ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.
“Tulikutana
si kujadili kiasi hicho cha fedha pekee, bali kutazama wajibu wa mamlaka ya
Jiji la Dar es Salaam kuwa waangalizi namba moja wa mifumo ya usafiri na
haki za abiria jijini humo,” alisema Mbowe.
Alitaja
wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Meya
wa Ubungo, Boniface Jacob, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Kinondoni,
Maulid Mtulia na Naibu Meya wa Ilala.
Hivi
karibuni kuliibuka mvutano kati ya Serikali na uongozi wa Jiji hilo
linaloongozwa na Ukawa kuhusu kuidhinisha mabilioni hayo ya uuzwaji wa hisa
asilimia 51 kati ya 100 kwa kampuni ya Simon Group.
Jumamosi
iliyopita, Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo chini ya Mwita kwenye kikao chake
cha kawaida lilishindwa kufikia mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kwa
kilichoelezwa kuwa ni sawa na kubariki ufisadi wa uuzwaji wa hisa hizo ambazo
wanaona ni kiasi kidogo.
Kikao
hicho kilifanyika kutokana na agizo la Rais John Magufuli Januari 27 wakati
akizindua mradi wa mabasi yaendayo haraka.
Katika
agizo hilo Rais alitoa siku tano kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha kiasi hicho
cha fedha kinapangiwa matumizi.
“Tumelitazama
hili kwa upana na kwa kina zaidi, tumekubaliana kuunda kamati ya watu watano
ambayo itakuwa ikiripoti kwangu, itakwenda kuandaa mpango mkakati wa namna ya
kuboresha usafiri wa Dar es Salaam,” alisema Mbowe.
“Mapendekezo
ya kamati yakikamilika ndani ya wiki moja au mbili, tutayawasilisha serikalini
na imani yetu watayapokea kwani Dar es Salaam ni ya wote, leo inaongozwa na
Ukawa sijui kesho itaongozwa na nani. Tunapaswa kuweka kando siasa na kutanguliza
maslahi ya Taifa.”
0 comments:
Post a Comment