*Ni kwa tuhuma za kujihusisha na mihadarati
*Operesheni ndani ya familia na kaya kuanza
Hussein Ndubikile
Wema Sepetu kituo cha Polisi cha Kati |
MSANII wa maigizo, Wema Sepetu (28) na
wengine 11 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kwa tuhuma mbalimbali za
matumizi ya dawa za kulevya.
Mbali na Wema aliyekuwa Mnyange wa
Tanzania mwaka 2006, watuhumiwa wengine ni Hamidu Chambuso, Rajab Salum, Romeo
George, Khalid Mohamed ‘TID’, Lulu Shilengwa, Said Masoud na Nassoro Nassoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema baada ya kuwahoji, 11
walikiri kujihusisha na dawa hizo huku akieleza kuwa Wema na Omari Micheni(32)
walikana ndipo polisi walipowafanyia upekuzi wanakoishi na kuwakuta na misokoto
ya bangi.
“Tunaendelea vizuri na opereshani ya
kupambana na dawa za kulevya, ndani ya siku tatu tumekamata kete 299 bado hazijathibitika
ni dawa za aina gani mpaka zitakapopelekwa kwa Mkemia Mkuu,” alisema.
Alisema baada ya kuwapekua Wema na Omari
walikutwa na misokoto hiyo huku mwenzake alikutwa na kete tano za bangi na
kwamba wasanii hao wataandaliwa mashitaka na kupelekwa mahakamani.
Hata hivyo, Sirro alisema watuhumiwa hao
11 watafilishwa kiapo baada ya kukiri kutumia dawa hizo.
Kamanda Sirro alisema hakuna mtuhumiwa aliyeonewa
kwani yeye ndiye alichukua jukumu la kuwahoji na watuhumiwa walikiri kutumia
dawa za aina ya heroine, bangi na kokeini, hivyo kusaidia kutaja watu
wanaowauzia.
Aliongeza kuwa watuhumiwa waliokiri
watafikishwa mahakamani kula kiapo kitakachoombwa na Polisi ambacho kitawaweka
chini ya uangalizi wa Polisi kwa miaka miwili wakitakiwa kuripoti mara mbili
kwa mwezi na kuahidi kuacha tabia hiyo.
Pia alisema polisi walikamata puli ya
misokoto mikubwa 104 na kete 107 za bangi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku 10 kwa wenyeviti wa Mitaa kutoa taarifa
za nyendo za wanaojihusisha na matumizi na biashara ya mihadarati.
Ameonya kuwa wasipofanya hivyo
wataunganishwa kwenye kesi za watuhumiwa watakaokamatwa kwenye mitaa yao.
Mkuu wa Mkoa pia alitoa siku 10 kwa wazazi na walezi kutoa
taarifa kwenye madawati ya upelelezi, za watoto wao endapo wanajihusisha na
dawa hizo.
Aliwataka wanaotumia na wanaofanya
biashara ya dawa hizo wajisalimishe Polisi kabla hawajachukuliwa hatua za
kisheria.
Aliitaka jamii kutambua kuwa Rais John
Magufuli hataki kusikia biashara na matumizi ya dawa hizo, hivyo wajue kuwa
mapambano haya si ya mtu mmoja.
0 comments:
Post a Comment