Suleiman Msuya
Khamis Mgeja
|
MWENYEKITI wa Taasisi ya Tanzania
Demokrasia Foundation, Hamis Mgeja, amesema nchi inaendeshwa kwa matukio, hali
ambayo inayotishia kuchelewesha jitihada za maendeleo na kukuza uchumi.
Mgeja alisema hayo jana wakati
akizungumza na JAMBOLEO, ambapo alibainisha kuwa huu ni wakati wa kujikita
katika uvumbuzi na utafiti utakaosaidia kuendeleza nchi.
Alisema iwapo utaratibu huo wa kuendesha
nchi kwa misingi ya matukio utaendelea, ni dhahiri jitihada za kuchochea
maendeleo zitakwama kutokana na matukio hayo kuchukua muda mrefu.
Mwenyekiti huyo alisema iwapo mfumo au
utaratibu huo unaoonekana kugusa maslahi ya mtu mmoja mmoja utapewa nafasi
katika kuongoza nchi, hauwezi kutatua changamoto zilizopo na kutaka mamlaka husika
kuelekeza nguvu katika ubunifu na utafiti wa kuondoa umaskini.
Mgeja alisema umefika wakati kwa
viongozi wastaafu hasa marais na viongozi wa dini, kushauri kuhusu misingi ya
uongozi, itakayogusa maslahi ya watu wote bila yoyote kuona anaonewa.
Alisema Tanzania ni nchi ya kila mtu na
hakuna mtu yoyote mwenye hati miliki, hivyo dhana ya kuheshimiana inahitajika.
Mwenyekiti huyo alisema inasikitisha
kumuona Rais mstaafu Benjamin Mkapa, akijikita katika utatuzi wa migogoro ya nchi
zingine, huku Tanzania ikiwa na viashiria vya watu kutokubaliana na chuki
zikiongezeka.
“Kwa sasa hali ya nchi inaonekana
imezingirwa na giza kwani wananchi hawajui wanaelekea wapi hasa katika misingi
ya kidemokrasia, nchi inaenda kwa matukio na si kwa uvumbuzi,” alisema.
Mgeja alisema kwa hali ilivyo sasa,
hakuna mtu aliye salama kwani ni jambo la kawaida kukuta mtu leo ameitwa Polisi
au amekamatwa bila hoja za msingi.
Akizungumzia changamoto zinazotokea kwa
sasa, alisema zinatokana na kukosekana kwa viongozi walioandaliwa kama
alivyofanya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Mwalimu alizingatia misingi ya kuandaa
viongozi hali iliyochangia uadilifu na kuheshimiana kati yao, hivyo uamuzi wa
viongozi walioandaliwa kuachwa, ndio matokeo yanayoonekana sasa,” alisema.
Mgeja alisema pamoja miongoni mwa changamoto
zilizo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilizochangia waondoke ilikuwa kukiukwa
kwa misingi iliyojengwa na Mwalimu.
Kuhusu dawa za kulevya, alisema hilo ni
tatizo la kidunia linalohitaji umakini wa hali ya juu pamoja na uchunguzi na
kusema anamuunga mkono Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa
za Kulevya, Rogers Siyanga, ambaye ameweka bayana kuwa atazingatia misingi ya
sheria katika kufanya kazi hiyo.
0 comments:
Post a Comment