Emeresiana Athanas
Dk Susan Kolimba |
WATANZANIA 132 wamekamatwa na kufukuzwa
nchini Msumbiji wakituhumiwa kuishi bila kufuata taratibu za uhamiaji.
Watanzania hao wamekamatwa mjini Monte
Puez jimboni Cabo Delgado kwenye operesheni maalumu ya kuwakamata na
kuwarudisha kwao raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kinyume cha taratibu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dk Susan Kolimba, alisema kutokana na tukio hilo ubalozi wa Tanzania nchini humo
umefika eneo hilo kufuatilia na kujionea hali halisi.
"Sisi si kwamba tunapingana na
mchakato huo, lakini tunafuatilia ili kujua kama raia hao wanatendewa haki na
wanatolewa kihalali kwani tumepata malalamiko kwamba wapo walionyang'anywa pasipoti
zao na kunyanyaswa," alisema.
Alisema ubalozi unaendelea kufanya
mawasiliano ya kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa
Watanzania na mali zao na kinachofuata kuwahusu.
"Kuna baadhi ya maofisa wa Serikali
wakiwamo wa Uhamiaji wamefika maeneo hayo ili kubaini haya ambayo Watanzania
hao wamesema ikiwamo kunyang'anywa pasipoti na mali zao, ili tujue kama ni
kweli ili tukae na Serikali ya Msumbiji kujua nini cha kufanya," alisema.
Alisema Watanzania wapatao 3,000 wanaishi
na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii mjini Monte Puez na tangu operesheni
hiyo ianze, raia 132 wamerudishwa nchini.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka
Watanzania waishio ughaibuni, kufuata sheria na taratibu za nchi wanamoishi.
0 comments:
Post a Comment