Aidan Mhando, Mwanza
Mama Samia Suluhu |
MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu ametaka
wataalamu wa Sayansi na watafiti Afrika Mashariki, kutumia Kongamano la Utafiti
wa Kisayansi la Bonde la Ziwa Victoria kujadili na kutoka na majibu yatakayosaidia
kutunza rasilimali za Ziwa hilo.
Akizungumza mjini hapa jana, akifungua Kongamano hilo la siku mbili lililojumuisha viongozi
wa nchi za Afrika Mashariki, wadau wa Sayansi, watafiti na wakazi wa Mwanza, Makamu wa Rais alisema
Ziwa Victoria linakabiliwa na changamoto nyingi, lakini zinaweza kupatiwa
ufumbuzi kupitia kongamano hilo.
“Mkutano huu ni muhimu kwa nchi zetu za
Afrika Mashariki ambamo Ziwa Victoria limo. Kuna changamoto nyingi ambazo
zinalikabili, hivyo kupitia kongamano hili tunaweza kujadili njia sahihi za
kutafuta ufumbuzi,” alisema Samia.
Alisema Ziwa Victoria ni chanzo kikuu
cha uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki, hivyo inahitajika mikakati sahihi ya
kulisimamia ikiwamo utunzaji samaki wanaopatikana na rasilimali nyingine zilizopo
ndani ya Ziwa hilo.
“Ziwa Victoria ni la kihistoria. Lina msaada
mkubwa wa kiuchumi katika nchi zetu, linasaidia upatikanaji huduma za maji,
hivyo uwepo wake ni muhimu tuendelee kulitunza vizuri kitaalamu ili liendelee
kunufaisha nchi zetu,” alisema.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Greyson Lwenge
alisema wanasayansi na watafiti wanaweza kuanzisha maendeleo endelevu ya
kufanyia utafiti katika Ziwa hilo, ili kusaidia utunzaji wa rasilimali
zilizopo.
“Changamoto kubwa kwa Ziwa Victoria ni
uchafuzi wa mazingira unaotokana na magugumaji. Mabadiliko ya tabianchi pia ni
changamoto ya utunzaji mazingira, hivyo watafiti na wanasayansi watasaidia
utunzaji wa Ziwa na raslimali zilizopo,” alisema Lwenge.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Balozi Augustino Maiga alisema Ziwa Victoria ni kitambulisho thabiti
cha nchi za Afrika Mashariki na lina historia ndefu, hivyo ni muhimu likatunzwa
vizuri.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la
Ziwa Victoria, Ally Matano alisema lengo la kongamano hilo, ni kukutanisha
wanasayansi kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazolikabili Ziwa hilo ambalo ni
chanzo kikuu cha uchumi.
0 comments:
Post a Comment