Charles James
IMAMU Mkuu wa Msikiti wa Swiratwal
Mustaqima, Shekhe Haroun Matambo, amesema njia inayotumika kutaja majina ya watu
katika vita dhidi ya dawa za kulevya, si sahihi na hata kitabu kitakatifu cha
Quran kinakataza.
Akizungumza kwenye mawaidha ya Ibada ya
Ijumaa jana kwenye msikiti huo Mabibo, Dar es Salaam, Shekhe Matambo aliunga
mkono vita hivyo lakini akakosoa kuwa utaratibu unaofanyika sasa wa kutaja
majina kabla ya uchunguzi haufai.
Kauli hiyo imekuja wakati vita
iliyoanzishwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
ikipamba moto dhidi ya watuhumiwa wa uuzaji na utumiaji wa dawa hizo, huku watu
wa kada mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wanasiasa, wafanyabiashara na
wasanii wakitajwa.
Shekhe Matambo alisema vita dhidi ya dawa
za kulevya si ya nchi moja pekee bali ni ya kimataifa, lakini akashauri ni vema
sheria na utaratibu wa kupambana na watu hao vikafuatwa.
Alisema njia ya kutaja majina ya watu si
nzuri, kwa sababu Serikali inaweza kujikuta ikipoteza fedha nyingi kulipa
waliotuhumiwa endapo watashindwa kuwasilisha vielelezo vya ushahidi kujihusisha
na dawa hizo.
“Hata kitabu cha Quran kwenye Surat
Hujirat aya ya sita, Mwenyezi Mungu anasisitiza kuwa usiifanyie kazi haraka
habari ambayo umeletewa na mtu bila kuifanyia uchunguzi na upelelezi, ili usije
kumvunjia mtu heshima yake mbele ya jamii ambayo inamwangalia.
“Serikali ndiyo yenye mamlaka, kama wana
majina ya watu wanaojihusisha na biashara hii haramu, wangewaita kimyakimya na
kuwahoji wakiwa tayari na vidhibiti, kisha wawapeleke mahakamani lakini kwa
njia hii wanaweza wakajikuta wanalipa watu fidia nyingi baada ya kuharibu majina
yao,” alisema Shekhe Matambo.
Alisema yeye na Waislamu wengine
wanaungana na Serikali katika vita hivi lakini akasisitiza kuwa ni vema
utaratibu mzuri ukatumika ili usije kuumiza watu huku akisema kipo kitengo
maalumu cha kupambana na dawa za kulevya, ambacho kilipaswa kushughulika na
watu hawa na si hali hii inayoendelea.
“Nampongeza ndugu yangu Kamanda Sirro
(Simon), juzi nilimsikia hata yeye akisema inawezekana wapo watu wana visasi
vyao, hivyo wakawa wanachongeana matokeo yake mmoja akaumia hivyo akasisitiza
watu wawe na uhakika na habari wanazotoa kwa Jeshi hilo, hiyo ni kauli nzuri na
ninaiunga mkono,” alisema Shekhe huyo.
Shekhe Matambo alitoa mwito kwa Serikali
kushirikiana na viongozi wa dini katika kukabiliana na vita hivi huku akitaka
busara, hekima na utaratibu wa kisheria kufuatwa bila kuharibu heshima za watu.
Pia alisema anaungana na wabunge
waliotaka Serikali ifute biashara ya michezo ya kubahatisha (BET) kutokana na
kuharibu kundi kubwa la vijana ambao wanaacha shule na wengine kuiba fedha
majumbani mwao ili wakacheze.
“Napingana na Naibu Waziri wa Fedha, Dk
Ashantu Kijaji ambaye alisema Serikali haiwezi kufuta kubeti kwa sababu kunaiingizia
Serikali faida kubwa, anapaswa kufanya uchunguzi yakinifu kati ya faida
inazopata Serikali na athari ambayo jamii inakumbana nayo kwa mchezo huo.
“Mwenyezi Mungu anasema kwenye Quran
sura ya tano, kwamba kila mtu afanye kazi na si kupata fedha kwa njia haramu,
na hata Rais Magufuli anasisitiza watu wafanye kazi na si kubeti kama Dk Kijaji
anavyotaka kutuaminisha,” alisema Shekhe Matambo.
Alisema Serikali inapaswa kupambana na pombe
za viroba ambayo vimegeuka sumu kwa vijana na wengi wamejiingiza kwenye ulevi
huo, kwa sababu kwanza upatikanaji wake ni rahisi kwa maana ya bei.
“Viroba vimekuwa tatizo kwa asilimia
kubwa ya vijana hasa madereva bodaboda, wanakunywa sana na h i inasababisha
ajali nyingi barabarani, lakini pia kuua nguvukazi ya Taifa ambapo vijana ndilo
kundi kubwa linalotegemewa kufanya kazi ili kuifikia Tanzania ya viwanda inayotakiwa
na Rais Magufuli,” alisema Shekhe Matambo.
0 comments:
Post a Comment