Sharifa Marira
Profesa Joyce Ndalichako |
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amesema Serikali inatarajia kuajiri walimu wa
masomo ya Sayansi zaidi ya 4,000 ili kupunguza uhaba wa walimu hao nchini.
Profesa Ndalichako alisema hayo juzi kwenye
ziara yake wilayani Rufiji akieleza kuwa kipaumbele kitatolewa kwa shule za
wilaya hizo, ambazo kila aliyotembelea alikuta uhaba wa walimu hao na zingine kutokuwa
nao kabisa kwa miaka zaidi ya mitano.
Akiwa katika Sekondari Utete akifuatana
na Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM) alieleza kusikitishwa na kufeli
kwa wanafunzi wengi wa kidato cha nne mwaka jana na kuwaeleza kuwa Serikali
itajitahidi kutatua changamoto zilizopo ili wanafunzi wasipate kisingizio cha
kufeli.
“Jitihada za Mbunge wenu anavyowaongelea
bungeni, zimenileta hapa leo kutokana na Serikali kuwa sikivu lakini nimesikitishwa
na matokeo yenu ya mwaka jana, mmefeli sana lakini nimeona changamoto zilizopo
shuleni kwenu ukiwamo ukosefu wa walimu hasa wa Sayansi, kuhusu vifaa vya
maabara tutawaletea mwezi huu na uchakavu wa vyoo tutajitahidi kurekebisha,”
aliahidi Ndalichako.
Aliasa wanafunzi kutochanganya mambo na
kuendekeza ngoma, muziki au mapenzi kwani mambo hayo yanachangia kiasi kikubwa
wanafunzi kufeli.
Mchengerwa aliwataka wanafunzi
kujibidiisha na masomo kwa kuwa katika kipindi cha uongozi wake anajitahidi
kuishawishi Serikali kuboresha elimu ili kuzalisha wasomi wengi ambao wataendeleza
wilaya yao.
Aliipongeza serikali kwa kusajili shule
ya Umwe ambako wanafunzi walikuwa na shida kusoma shule mbili tofauti kwa kuwa
hawakuruhusiwa kufanya mitihani katika shule ambayo haijasaliwa na kilichobaki
ni kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
0 comments:
Post a Comment