*Spika Ndugai asema kila kitu kiko tayari
*Mbunge
amwomba JPM avunje Bunge
Waandishi Wetu
WABUNGE wamemshukia Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda, juu ya kauli yake ya kutaka wawakilishi hao wa wananchi
kupimwa ulevi.
Wawakilishi hao wamebainisha kuwa matamshi
tata ya mteule huyo wa Rais yanaashiria yanawafanya wanamvutia pumzi hadi Bunge
lijalo ili ajieleze kwao.
Wakati wabunge hao wakieleza hayo, Spika
wa Bunge, Job Ndugai amesema hawezi kumjibu Makonda kwani ni mapema mno na
taratibu zinafanyika kumwita bungeni.
Akitoa maoni yake kuhusu Makonda, Mbunge
wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Msukuma alikwenda mbali zaidi na kubainisha
kuwa kama inaonekana wabunge hawatekelezi vyema majukumu yao, Rais John Magufuli
avunje Bunge.
Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, pia alibainisha
kuwa taratibu za kuhakikisha Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander
Mnyeti wanahojiwa na Bunge kwa kutoa kauli za kuingilia haki na madaraka ya mhimili
huo, zipo katika hatua nzuri.
Makonda alitoa kauli hiyo juzi Dar es
Salaam katika hafla maalumu ya kumkabidhi orodha mpya ya watuhumiwa wa biashara
ya dawa za kulevya na kumkaribisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya, Rodgers Siyanga.
Katika hafla hiyo, Makonda alimkumbusha
Ndugai kutekeleza kauli yake ya Mei mwaka jana bungeni, kuhusu kusudio lake la
kuanza kuwapima wabunge ili kubaini kama wanatumia ulevi kabla hawajaingia
ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Katika maelezo yake, Msukuma alisema
kauli zinazotolewa na Makonda zinalidhalilisha Bunge, akiwamo Waziri Mkuu
ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni.
“Anavyosema wabunge wapimwe maana yake
hata Majaliwa naye anapaswa kupimwa kama anatumia dawa ama la! Ina maana hata
Ndugai naye anapaswa kupimwa? Huku ni kulitukana Taifa maana wabunge
tumechaguliwa na wananchi,” alisema Msukuma.
“Ina maana sisi (wabunge) tukipimwa kwa
kuhisiwa kuwa tunatumia dawa maana yake wananchi wamechagua wabwia ‘unga’.
Makonda amedhalilisha Taifa,” alisema.
Mbunge huyo ambaye alimshambulia Makonda
katika mkutano wa sita wa Bunge uliomalizika Ijumaa iliyopita, alisema wabunge
watapambana kwa kauli hiyo katika Bunge lijalo.
“Rais analihutubia Bunge ina maana na
yeye anakuja kuhutubia ‘mateja’…, kama inaonekana Bunge halifanyi kazi yake
vizuri basi Rais alivunje kuliko kudhalilisha wabunge,’’ alisema Msukuma.
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche
(Chadema) alisema, “siamini kama Makonda anafanya mambo haya maana anajua
majukumu yake kulingana na wadhifa wake. Lazima tujiulize nani yuko nyuma yake,
anayemtuma lengo lake nini?”
Alisema haiwezekani kwa Mkuu wa Mkoa
kujiamini kulishambulia Bunge, wabunge na kuhoji mamlaka ya chombo hicho cha
Dola bila kuwa na watu nyuma.
“Bunge ni chombo kikubwa sana na kina
kiongozi wake, kama Makonda anataka kushauri Bunge angeweza kumshauri Spika si
kukishambulia chombo hiki hadharani na kuwaaminisha watu kuwa Bunge si lolote
si chochote,” alisema Heche.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe
(ACT-Wazalendo) alisema Makonda anatakiwa kutekeleza majukumu yake na kuwaacha
wabunge kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Mkoa wa Dar es Salaam una changamoto
nyingi sana ikiwamo ya elimu baada ya shule sita kati ya 10 zilizofanya vibaya
mtihani wa kidato cha nne kutokea mkoani humo. Atatue hizo kwanza si kuingilia
mhimili mwingine,” alisema Zitto.
Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo
(Chadema) alisema, “Makonda hajui chochote kwa nafasi aliyonayo. Hana mamlaka
yoyote ya kumwomba au kumwagiza Spika na kama atafanikiwa hilo ipo siku
ataagiza Mahakama
kupima majaji na mahakimu.”
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa
(Chadema) alisema Mkuu wa Mkoa hana weledi katika utendaji wake wa kazi.
“Kuendelea kumjadili ni kupoteza muda,
maana kuna mambo mengi ya msingi ya kujadili yanayohusu wananchi. Tukiendelea
kumjadili tunampa umaarufu wa bure ni mtu,” alisema.
Kuhusu Makonda kumkumbusha Ndugai juu ya
wabunge kupimwa alisema, “hajui mipaka yake ya kazi anaingilia majukumu
yasiyomhusu.
“Naunga mkono vita vya dawa za kulevya ila
tatizo langu ni kauli za Makonda hasa kuingilia majukumu ya Spika…, kukumbusha
kwa namna ile ni kuagiza! Spika hapewi maagizo anatekeleza mambo
aliyoyaanzisha.”
Makonda, Mnyeti
Jumatano iliyopita Bunge lilipitisha maazimio
manne likiwamo la kuitwa kwa wateule hao wa Rais baada ya kutoa kauli za
kuingilia madaraka ya chombo hicho jambo ambalo Ndugai alisema taratibu zinaendelea,
taratibu zikikamilika vyombo vya habari vitajulishwa.
0 comments:
Post a Comment