Moses Ng’wat, Kyela
MKUU wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta,
amewaagiza madiwani, watendaji wa kata, vijiji na viongozi wengine wenye
dhamana katika maeneo yao kuhakikisha wanajihusisha kikamilifu kusimamia na kutoa
elimu dhidi ya mauaji holela yanayotokea baada ya watu kujichulia sheria
mkononi.
Kitta ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hiyo, amelazimika kutoa agizo hilo, baada ya
takwimu za makosa ya kujichukulia sheria mkononi wilayani humo kuonyesha kuwa,
katika kipindi cha miezi miwili watu watano wameuawa na wengine kujeruhiwa.
Akitoa salamu za Serikali katika kikao
cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, Kitta alisema matukio
hayo hayakubaliki na yanapaswa kukomeshwa mara moja kwa viongozi wote waliopewa
dhamana kuhubiri amani.
“Niombe madiwani katika maeneo yenu
hakikisheni mnasimamia amani ili kuepusha watu kujichukulia sheria mkononi na
kukatisha uhai au kujeruhi watu wengine wanaowatuhumu kuwa ni wakosefu kana
kwamba wana haki ya kufanya hivyo,” alisisitiza Kitta.
Alisema ndani ya miezi miwili ya Desemba
2016 na Januari mwaka huu, takwimu zinaonyesha kuwa watu watano uhai wao
umekatizwa kutokana na tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi na wengine
kadhaa kujeruhiwa.
“Hakuna mtu mwenye haki ya kutoa uhai wa
mtu mwingine au kujeruhi hata kama
amekosa, watuhumi wanatakiwa kufukishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria
ichukue mkondo wake, hivyo elimisheni watu kuacha vitendo hivyo na watakaobaini
hatua kali zitachukuliwa”.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema ukiachilia
mbali mauaji ya watu hao watano ndani ya miezi miwili, hivi karibuni mtu mmoja
ambaye hata hivyo hakumtaja jina alijeruhiwa na kusababisha kung’olewa jicho
baada ya wananchi kumshambulia katika vurugu zilizotokana na vijana wa kata ya
Matema.
Kutaka kulazimisha kupewa ajira katika
kampuni ya ujenzi ya kichina inayojenga barabara ya Kikusya hadi Matema,
wakiutuhumu uongozi wa kampuni hiyo kufanya upendeleo kwa kuajiri vijana wengi
kutoka nje ya Wilaya hiyo.
“Inasikitisha sana, Yule kijana
nimeonana naye hivi sasa kapoteza jicho lake kwa sababu za watu kufanya mambo
bila kujali sheria, hata kama wale wachina wamefanya hivyo, wananchi
hawakupaswa kufanya kile walichofanya”.
0 comments:
Post a Comment