Charles James
WAVUVI wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa wamegoma
kuvua samaki wakipinga nyanyaso kutoka kwa Serikali kuhusu utata wa kipimo cha
urefu wa nyavu kinachopaswa kutumiwa.
Wavuvi hao wameamua kugoma baada ya
mfululizo wa vitendo wanavyodai kuwa ni vya uonevu kutoka kwa maofisa wa uvuvi
na askari wa doria jijini Mwanza wanaowakamata kwenye operesheni zao za usiku
ziwani.
Hivi karibuni wavuvi 14 walikamatwa Bugogwa,
Igombe, wilaya ya Ilemela na kunyang’anywa nyavu zao zinazokadiriwa kuwa na
thamani ya Sh milioni 50.
Akizungumzia suala hilo la mgomo, Mbunge
wa Viti Maalumu Suzan Masele alisema athari za mgomo huo zimeanza kuonekana
kuanzia kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea samaki kwa kitoweo au biashara za
mama ntilie, lakini pia kwa viwanda vya samaki vinavyozalisha kwa kutegemea
samaki wanaovuliwa na wavuvi hao.
“Kinachoshangaza badala ya Serikali
kujikita kujadili njia za kutatua mgogoro huo kwa kukutana na wavuvi na
kuwaelimisha juu ya urefu wa nyavu unaotakiwa, wamesema wanaunga mkono mgomo
huo kuendelea ili kusaidia samaki kuzaliana,” alisema Suzan.
Alisema kauli hiyo imethibitisha kuwa
Serikali ya Mwanza imeshindwa kuangalia athari wanazopata wananchi kutokana na
mgomo huo na endapo utaendelea bila ufumbuzi wa haraka utadhihirisha kuwa
Serikali ya Mkoa imeshindwa kutekeleza majukumu yake.
“Tumewasikia wavuvi kupitia vyombo vya
habari wakisema wako pamoja na Serikali kupinga uvuvi haramu hasa wa makokoro
na milipuko na wako tayari kusaidiana kuwapata na kuwadhibiti wanaofanya
vitendo hivyo, sasa kwa nini wasikae nao na kuwasikiliza?” Alihoji Mbunge huyo.
Alitoa mwito kwa Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi kuingilia kati na kumaliza mgogoro unaoendelea baina ya wavuvi
hao na Serikali ya Mkoa ili kusitisha mgomo wao kabla athari hazijawa kubwa.
0 comments:
Post a Comment