Mashaka Mgeta
ACHA NIPAYUKE
Mashaka Mgeta |
MWAKA 1994, Serikali iliyoongozwa na Rais wa awamu ya
tatu (mstaafu), Benjamin Mkapa, ilianza maandalizi ya kuandaa Dira ya Maendeleo
ya Taifa kwa utekelezaji wa utakaofikia kikomo chake mwaka 2025.
Miaka mitano baadaye, yaani 1999, dira hiyo ilizinduliwa.
Dira hiyo inajikita katika kusudio la kwamba ifikapo 2025, Tanzania iwe imepiga
hatua zisizokuwa za kawaida katika mageuzi ya uchumi na maendeleo, ili kufikia
hadhi ya kuwa taifa lenye kipato cha kati.
Miongoni mwa sifa stahiki kwa nchi itakapofikia hatua
hiyo ni pamoja na ukuaji wa viwanda, kuhimili ushindani wa kiuchumi, maisha
bora kwa wananchi, utawala wa sheria na kuwa na jamii iliyoelimika.
Unapoisoma Dira hiyo ambayo utekelezaji wake unahusisha
mpango wa maendeleo wa miaka mitano, unaweza kubaini maeneo machache
yaliyoainishwa, lakini yanayohitaji nyenzo, ushirikishi, rasilimali na uwezo wa
kutambua, kutathimini na kupanga namna tofauti za utekelezaji wake, ili kufikia
kusudio mahususi.
Unapoyapitia ‘maeneo’ kama ukuaji wa viwanda, kuhimili
ushindani wa kiuchumi, maisha bora, utawala wa sheria na kuwa na jamii
iliyoelimika ni rahisi kuyahesabu.
Lakini mipango, utekelezaji na kupima matokeo ni namna
nyingine inayohitaji ushiriki mpana wa Taifa na washirika wake.
Ninatambua kwamba mipango kama ule wa miaka mitano na
mikakati mbalimbali imewekwa ili kukidhi mahitaji ya Dira ya Maendeleo ya
Taifa. Hoja ni je, hivi sasa Taifa lipo kwenye njia sahihi ya kufikia kusudio
mahususi la dira hiyo?
Kupata jawabu sahihi la hoja hiyo kunahitaji kujielekeza
katika utekelezaji wa kila sekta kwa mujibu wa majukumu na wajibu wake,iwe ni
kwa upande wa umma na sekta binafsi.
Kupata jawabu sahihi kunahitaji kupima ushiriki wa
Serikali katika kutimiza wajibu wake wa kuweka mazingira rafiki na yanayovutia
uwekezaji, ushiriki wa umma na uboreshaji wa elimu utakaolifanya taifa kuwa na
watu wenye uelewa mpana wa kupanga, kuchambua na kutathimini masuala tofauti ya
kijamii.
Pia yapo mambo mengine kama uhuru wa habari na kujieleza,
mgawanyo wa utendaji kazi kwa mihimili ya Taifa, ukuaji wa sekta binafsi
inayoongoza kwa utoaji wa ajira na tegemeo katika uanzishaji wa viwanda.
Lakini yote hayo na mengine ambayo hayatajwa katika hoja
hii, yanapaswa kuwa kwenye fikra za Watanzania, wakiitumia mipango na mikakati
mingine kama nyenzo ya kufikia utekelezaji wenye tija wa dira hiyo.
Kwa hali ilivyo sasa, ingawa kwa kuzingatia ushahidi wa
ki-mazingira, sehemu kubwa ya jamii katika sekta tofauti ni kama imeiweka kando
Dira hiyo na sehemu za utekelezaji wake.
Mijadala inayohusu maendeleo na ustawi wa nchi na watu
wake ni kama inaelekea ‘kufa’. Viongozi wachache wa umma hususan Rais John Magufuli,
wanajikita katika kulirejesha taifa katika hoja zinazohusu ‘maeneo’ hayo.
Ingawa ni hivyo, Rais Magufuli pekee hawezi kufanikisha
nia ama kusudio kuu lenye kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa, bali ushiriki
mpana wa wasaizidi wake, wanataaluma, asasi za kijamii, vyama vya siasa,
taasisi za kidini, vyombo vya habari na kada nyingine.
Kwa mfano, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta)
lilipotangaza matokeo ya kidato cha nne kwa waliohitimu mwaka jana, kuliibuka
changamoto nyingi zinazoigusa sekta ya elimu, ikiwamo kuzidi kufanya vibaya kwa
shule za sekondari za Serikali.
Changamoto nyingine ni ugumu wa wanafunzi kufaulu somo la
hisabati katika kiwango kilichofikia asilimia 18.12, kwa mujibu wa Katibu
Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa
kiswahili katika asilimia 77.75.
Ni nani hivi sasa anajadili kuhusu matokeo mabaya ya
kidato cha nne kwa wanafunzi waliokuwa wanasoma shule zinazomilikiwa na Serikali?
Uhalisia na hoja za wanafalsafa wakiwamo Frederick Hegel,
Aristotle, Plato na wengine, wamezungumzia umuhimu wa elimu katika kuifanya
jamii ‘kutoka katika giza’ na `kuingia kwenye mwanga’, yaani kutoka kwenye
ujinga kwenda kwenye welevu.
Unapofuatilia mijadala na matukio kwenye jamii, ni kama
mambo muhimu kwa ustawi wa nchi ‘yanafunikwa’ kwa mbinu za kuibua jambo, hoja
ama tukio, likafuatiwa na jingine, na jingine, jingine. Lililopaswa kuwa ajenda
na mjadala kwa jamii linasahaulika, maisha yanaendelea.
Zipo changamoto nyingine zinazochangia nyingi
zinazochangia kudumaa kwa huduma za kijamii kama afya, kilimo, viwanda,
biashara, ufugaji, maji nakadhalika.
Vipo vitendo vinavyohatarisha haki, usawa na usalama wa
watu na mali zao; kwa mfano kuibuka kwa vikundi maarufu kama ‘panya road’.
Kuwapo kwa mazingira magumu ya kufanya shughuli za kiuchumi hivyo kuchangia
biashara kadhaa kufungwa na waajiriwa wakarejea mtaani. Nani anayejadili hayo?
Taifa halina wataalamu wa uchumi, biashara, hifadhi ya
jamii, maendeleo na ustawi wa watu? Hakuna sekta binafsi? Changamoto hizo
zinazosikika kila kona nchi haziwafikii walengwa ili waishauri Serikali na kwa
ushirikiano wa pamoja ipatikane suluhu yenye tija kwa nchi na watu wake?
Wakati hayo yakitokea, Tanzania imeendelea kuwa nchi
mwanachama wa jumuiya za kikanda na kimataifa zinazoshirikiana katika nyanja
tofauti zikiwamo zile zinazozorota ndani ya nchi. Katika hali hiyo, Watanzania
watawezaje kumudu ushindani dhidi ya raia wa mataifa mengine?
Kwa maoni +255754691540
0 comments:
Post a Comment