Grace Gurisha
WASANII Wema Sepetu na Agnes Waya maarufu (Masogange)
jana walikutana uso kwa uso katika Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam, huku kila
mmoja akikabiliwa na kesi yake lakini zote zinahusu tuhuma za kutumia dawa za
kulevya.
Wema ambaye ni muigizaji wa filamu na Masogange,
mnenguaji licha ya kukutana kwa kesi zao, pia familia zao zilikutana
zikifuatilia mashtaka dhidi ya ndugu zao huku zikitajwa kuwa na uhasimu.
Wakati Wema akipanda ngazi za mahakama hiyo kwenda
kizimbani kwa ajili ya kusikiliza kesi yake kwa mara ya pili, Masogange alikuwa
akifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi wa askari mmoja wa kike.
Katika mahakama hiyo, Masogange (28), amepandishwa
kizimbani kwa mara ya kwanza akishtakiwa kwa mashtaka mawili ya kutumia dawa za
kulevya aina ya Heroin na Oxazepam.
Hata hivyo, Masogange alipata dhamana baada ya kusota
mahabusu siku nane wakati Jeshi na Polisi lilipomshikilia kwa mahojiano ya
tuhuma ya kujihusisha na dawa za kulevya.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Constantine
Kakula alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017
katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za
kulevya aina ya Heroin.
Katika shtaka la pili, Kakula alidai kuwa kati ya
Februari 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam, ambapo alifanya
makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha sheria ya kupambana na dawa za
kulevya namba 5 ya mwaka 2015.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Masogange alikana kuhusika
na tuhuma hizo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi
umekamilika au la.
Hakimu Mashauri alisema ili mshtakiwa awe nje kwa dhamana
anatakiwa awe na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atasaini bondi
ya Sh milioni 10 na mshtakiwa asitoke nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa
na kibali cha mahakama.
Hata hivyo, Masogange alikamilisha masharti hao na
kuachiwa kwa dhamana na kesi imeahirishwa hadi Machi 21,2017 kwa ajili ya
kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Wema anashtakiwa kwa tuhuma za kukutwa na msokoto mmoja
wa bangi na vipande viwili vidogo vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Wakili wa Serikali, Kakula alidai jana mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu Thomas Simba kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba
tarehe nyingine ya kutajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 15 mwaka huu kwa
kutajwa.
Mbali na Wema washitakiwa wengine ni wafanyakazi wake wa
ndani Angelina Msigwa (21) na Matrida Abas (16), ambapo wote wanashitakiwa kwa
kosa moja la kukutwa na kiasi kidogo cha dawa za kulevya.
Ilidaiwa kuwa Wema na wenzake walitenda kosa hilo
Februari 4, 2017 February mwaka huu, huko nyumbani kwao Kunduchi Ununio Wilaya
ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam walikutwa na misokoto hiyo.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, walikana kuhusika na
tuhuma hizo. Hakimu Simba alisema ili washitakiwa wawe nje kwa dhamana
wanatakiwa wawe na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini bondi ya Sh milioni
tano kwa kila mmoja.
Hata hivyo,Wema na wenzake walitimiza masharti hayo na
kuachiwa kwa dhamana, lakini kabla hawajatoka mahakamani Simba aliwataka
wahakikishe wasiruke dhamana pindi wanapotakiwa kufika mahakamani wafike.
0 comments:
Post a Comment