Salha Mohamed
Hashim Mgandilwa |
MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim
Mgandilwa, amesema wilaya hiyo ina wagonjwa wanne wa kipindupindu waliolazwa na 11
walitibiwa na kuruhusiwa kutoka hospitali.
Taarifa za ugonjwa huo zilitolewa Februari
18 mwaka huu baada ya mtu mmoja kufariki akiwa njiani kwenda hospitali baada ya
kulalamika maumivu ya tumbo.
Mgandilwa alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari ambapo alifafanua chanzo cha ugonjwa huo
wilayani humo.
Kwa mujibu wa Mgandilwa, ugonjwa huo
umetoka katika familia mbili zenye watu 15, ambapo hadi sasa wagonjwa 11
wameruhusiwa kutoka hospitali huku wanne wakiwa bado wapo katika hospitali ya Vijibweni
jijini humo.
“Kulikuwa na mtu mmoja alitoka Rufiji
msibani, alipofika akawa analalamika tumbo ndipo wakaamua kumpeleka hospitali lakini
kabla ya kufika, akafariki njiani,”alisema.
Alisema ndugu hao baada ya kuona ndugu
yao amefariki, walimpeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ili wafanye
taratibu za mazishi.
Alisema familia hiyo haikufahamu kama
ndugu yao amefariki kwa kipindupindu, bali waligundua baada ya kuumwa familia
nzima.
“Baada ya kuona hivyo, Manispaa
tumefanya juhudi za kuhakikisha ugonjwa huo hausambai ambapo tumefanikiwa kwani
tusingefanikiwa, tungekuwa na wagonjwa zaidi ya 50,”alisema.
Mgandilwa aliwataka wananchi kuweka
mazingira yao safi na kuchemsha maji ya kunywa, ili kuua vijidudu
vinavyosababisha maradhi.
“Wananchi watunze mazingira yao yawe
safi, wachemshe maji na si kunywa hivyo hivyo, lakini pia wapashe vyakula kabla
ya kula,”alisema Mgandilwa.
Mgandilwa alitaja maeneo yaliyoathirika kuwa
ni Kichangani na kubainisha kuwa hadi sasa wameshapiga dawa ili kuua vimelea
vya ugonjwa huo na kuondoa madhara.
“Hakuna shule iliyofungwa, watoto wangu wanakwenda
kama kawaida, tumepiga dawa na tunaendelea kutoa matangazo na elimu,”alisema.
0 comments:
Post a Comment