Salha Mohamed
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB)
imekusanya Sh bilioni 8 kati ya Januari hadi sasa kutoka kwa wanufaika wa mikopo
yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdulrazaq Badru alibainisha hayo jana alipozungumza na mwandishi wa
habari hizi Dar es Salaam.
Alisema ongezeko hilo lilitokana na
ziara kwenye kampuni na mashirika yenye wanufaika wa mikopo na kutoa ufafanuzi
wa namna ya kulipa fedha hizo.
“Fedha zote si tu zinatoka kwa wadaiwa
sugu bali kwa wanufaika wote na kipato kinapanda tofauti na Novemba hadi
Desemba ambacho kilikuwa Sh bilioni 6,” alisema.
Alisema ziara waliyofanya imeongeza ari
ya kulipa kwa kuwapa waajiri kiwango kipya cha asilimia ya kulipa ambacho ni 15%
badala ya 8%.
Badru alisema kiwango hicho kilichoanza kutolewa
Januari ni tofauti na kilichoelezwa awali cha asilimia nane.
“Pia tumehakikisha wanakatwa makato yao
kwa njia sahihi na waajiri wengi wameitikia mwito kwani walikuwa hawajui kiasi
cha kukata na wajibu wao kama waajiri,” alisema.
Alisema mwajiri alipaswa kujua na
kutambua mtu anapaswa kutoa taarifa zake kama alikopa, hivyo waliwafanyia
wepesi wa kulipa madeni yao.
Aliongeza kwamba wanaendelea kuwatafuta
huku akiwataka kujitokeza ili kulipa na kukwepa mkono wa sharia.
“Nia yetu si kupelekana mahakamani,
lakini kulipwa ili wengine wanufaike na mkopo, kwani wako wengi wanahitaji,
karibu wote tunaowapata wanalipa,” alisema.
Alisema wale ambao bado Bodi haijawafikia
wajitokeze kulipa, huku akibainisha kuwa hadi sasa wadaiwa hao wamepungua
kutoka 84,000 hadi 72,000.
“Tumejiwekea lengo hadi Juni, tuwe
tumewaondolea watu wote usugu, huku tukiendelea na mikakati ya siku zote kwa kutembelea
waajiri na kuhakikisha wanakatwa wanufaika na kuwasilisha,” alisema.
Alisema wataanza awamu ya pili ya kutoa
elimu kwa wanufaika na waajiri, ili kuelewa umuhimu wa kulipa fedha hizo na
kusaidia wengine ili kuongeza Mfuko wao.
Alisema utaratibu wa kutoa picha za
wadaiwa hao bado uko pale pale, kwani kuna taratibu chache wanatarajia kumaliza
hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment