Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta |
FEBRUARI 2, mwaka huu, Rais John Magufuli alihutubia
kilele cha Siku ya Sheria, akiweka wazi namna Mahakama iliyo sehemu ya mihimili
mitatu ya nchi, inayovyokabiliwa na changamoto lukuki.
Kabla ya ‘kuzimwaga’ changamoto hizo, Rais Magufuli
alitambua na kupongeza kazi nzuri zinazofanywa na Mahakama katika kuhakikisha
kila raia anapata haki kwa kadri inavyoainishwa kwenye matamko ya haki za
binadamu.
Ieleweke kwamba kwa muda mrefu sasa, Mahakama
inayotarajiwa kuwa kimbilio la wanyonge, imejikuta ‘ikichafuka’ kutokana na
watendaji wake hususani baadhi ya mahakimu na majaji kukosa uadilifu.
Watendaji hao wamedaiwa kwa nyakati tofauti
wakishirikiana na watu wenye mamlaka na nguvu za kiuchumi na kisiasa,
kuwakandamiza wanyonge wasiokuwa na uwezo kama wao.
Lakini hali haipo katika mtazamo huo pekee, wapo
watendaji wa Mahakama, hata kama ni kwa idadi ndogo, wanaotajwa kupanga na
kushiriki mbinu za kisheria, kuuza haki za watu na hujuma dhidi ya taifa kwa
ujumla.
Mbinu hizo zinadaiwa kufanyika katika hatua tofauti
ikianzia upelelezi, uundwaji wa mashtaka, ushahidi na mwenendo wa kesi. Wanaoistahili
haki wanaikosa.
Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zisizokuwa salama katika
mukhtadha wa haki za watu. Rais Magufuli anapozungumza na watendaji wa
Mahakama, anajiweka kando na unafiki, anasimamia ukweli akibainisha changamoto
zinazopaswa kutekelezwa na mhimili huo.
Anabainisha mbinu tofauti zinazotumika ‘kuharibu’
mashauri yaliyopo mahakamani, ikiwamo mtindo maarufu kama ‘kupaki kesi’, lengo
likiwa ni kufanikisha azma ya kuubadili ukweli kuwa uongo ama mwenye haki
kutoistahili.
Ni wazi kwamba Rais Magufuli ‘alivyojifunua’ kwa ukweli
na uwazi, akijielekeza katika utendaji kazi wao, majaji na mahakimu wanapaswa
kujitafakari.
Watumie ujasiri, taaluma na maadili yao kukwepa kila aina
ya shinikizo zinazowafanya washiriki katika ‘kuuza’ haki za watu ama hujuma kwa
taifa.
Akishamaliza kuelezea changamoto zinazoikabili Mahakama, akajitokeza
mjane aliye mkazi wa Tanga, Swahaba Shosi, akielezea namna wenye mamlaka na
nguvu za fedha wanavyoitumia mahakama kutaka kumpora haki zake.
Akifanikiwa ‘kuokolewa’ na Rais Magufuli baada ya askari
wa ulinzi na usalama kufanikiwa kumdhibiti asifikishe ujumbe alioukusudia, Shosi
akaeleza kwa kirefu namna watendaji wa umma ikiwamo Mahakama, na miongoni mwa
waliomo katika sekta binafsi, wanavyoshirikiana kupora haki zake.
Kwa kadri ya maelezo ya Shosi yanayogota kwenye msingi wa
kunyimwa haki ya kurithi mali za marehemu mumewe, akazitaja taasisi husika kuwa
ni pamoja na polisi, Mahakama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (CAG).
Kwa kadri Shosi alivyojieleza mbele ya Rais Magufuli, pasipo
kujikita katika hoja tofauti zilizotolewa na wanaojitambulisha kuwa ni miongoni
mwa watoto wa marehemu, ilidhihirisha wazi kuwa na uhakika wa kile alichokuwa akikiwasilisha.
Hilo linaweza kuwa si jambo la maana sana katika Makala haya,
isipokuwa ni vizuri kubaini kwamba uwasilishi wake uliakisi sehemu ya hoja za
Rais Magufuli dhidi ya udhaifu ama changamoto zinazoikabili Mahakama.
Haki za wanyonge zinapoiukwa na walio kwenye mamlaka hasa
katika jeshi la polisi, taifa haliwezi kubaki salama. Watu wake hawawezi kuwa
na furaha kwa kadri inavyopaswa.
Ndio maana (pengine) ‘akifunuliwa’ kwa namna ya pekee,
Rais Magufuli akakemea ‘uovu’ unaojitokeza kwenye Mahakama za ndani, kisha
dakika chache baada anajitokeza mjane anayelalamikia udhaifu kama uliotajwa na
Kiongozi Mkuu huyo wa nchi.
Ni kama kusema katika hili, Mungu alimuona Rais Magufuli
katika dhamira na utashi wake wa kusema na kuisimamia kweli. Kwamba yapo
mazingira ambapo Mahakama inatumika (kupitia watendaji wasiokuwa waadilifu ama
kwa shinikizo), kupora haki za watu.
Wapo walioamini kuwa Rais Magufuli ananukuu taarifa
zinazofikishwa kwake kutoka vyombo mahususi vilivyo chini ya ofisi yake.
Tafakari iliyopo ni kwamba, ilikuwaje siku ambapo Rais
Magufuli ameguswa kuikosoa Mahakama na kuionya isishiriki kupora haki za watu
ama hujuma dhidi ya uchumi wa nchi, akajitokeza Shosi akiwa na madai yanayounga
mkono hoja za Rais?
Kwa matukio hayo mawili, Mahakama katika ngazi zote,
inapaswa kujitafakari, kujitathmini na kupata mwelekeo mpya wa kuhakikisha
kusudio kuu la kuwapo kwake kati ya mihimili mitatu ya nchi, linafanikiwa.
Kama ilivyo kwa kila mhimili katika utawala wa nchi kuwa
na umuhimu wake, Mahakama ina wajibu mpana kwa dhamana inayoainishwa hata
kwenye ulimwengu wa kiroho, kwamba haki ya mtu inamstahili kila aliyeumbwa na
Mwenyezi Mungu.
Wakati Rais Magufuli akiibua hoja ambazo si rahisi kwa
wakuu wa nchi kuzitoa, Mahakama inapoingia katika uongozi wa Kaimu Jaji Mkuu,
Profesa Ibrahim Juma, isijipambanue na ‘kuzaliwa upya’.
Mahakama isimamie misingi ya haki, itende haki na kutoa
haki kwa watu wote pasipo kujali asili inayotokana na itikadi za kisiasa, dini,
kabila ama vinginevyo.
Kwa maoni: 0754691540
0 comments:
Post a Comment