Mashaka Kinaya, Tanga
Kamanda Benedict Wakulyamba |
WAHAMIAJI haramu 25 raia wa Ethiopia wamekamatwa na Polisi
wilayani hapa, wakati wakiwa kwenye magari wakisafirishwa kutoka Tarakea,
Kilimanjaro kupitia Korogwe hadi Mbeya, lengo likiwa ni kwenda Afrika Kusini.
Taarifa zilieleza, kuwa Waethiopia hao walikamatwa juzi
saa 11 jioni eneo la Kiloza, Magila Gereza, wakisafiri kwa magari mawili aina ya
Toyota Land Cruiser.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Benedict Wakulyamba, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, huku
akibainisha kuwa wahamiaji hao wanatarajiwa kukabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji
ili taratibu zingine za kisheria ziendelee.
Waethiopia hao walikuwa wakitoka Tarakea, Kilimanjaro
kupitia Korogwe lengo likiwa kufika Mbeya ili kuendelea na safari yao kwenda Afrika
Kusini.
Pamoja na wageni hao kukamatwa, pia madereva Watanzania
Mkwawa Emily (40), David Meshack (36) na utingo Nelson Joseph (36) wote walishikiliwa
kwa muda Polisi Korogwe kwa mahojiano kabla ya kuletwa mjini hapa kwa taratibu
za kisheria.
Magari yaliyohusishwa na tukio hilo ni aina ya Toyota
Land Cruiser namba T 892 ASH likiendeshwa na Emily na utingo Joseph lililokuwa
na Waethiopia 11 na lililokuwa likiendeshwa na Meshack namba T 646 CKS likiwa
na wahamiaji 14.
Wahamiaji hao na umri wao kwenye mabano ni Almayu Kudra (22),
Beranu Tudasa (20), Mulegat Yufuma (29), Eyasu Damasha (23), Mulak Morau (26), Feker
Mator (26), Eyasu Turfa (25),Takatal Wudal (27), Salum Marekue (25), Tomoroa
Bagojam (20), Avinto Tuwili (19) na Hajira Ibrahim (20).
Wengine ni Malya Tala (20), Zayne Ketbo (22), Masfn Zamde
(22), Abrmi Digamo (25), Milatu Bachar (21), Lomibise Bolol (22), Lama Loba
(24), Ababa Tamile (26), Tamilat Hylee (26), Basmi Fonte (32), Tigante Ababa
(15), Dassan Tumiso (18) na Labi Lode (18).
Kukamatwa kwa wageni hao kulimfanya Mkuu wa Wilaya ya
Korogwe, Robert Gabriel kusema kuwa ipo haja kwa wananchi kuendelea kutoa
ushirikiano wa hali na mali kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Gabriel alisema wananchi wanapomhisi au kumtilia shaka
mtu kwenye eneo lao kuwa si mwenyeji waitaarifu Polisi na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama hatua ambayo itawezesha wahusika kukamatwa kwa mahojiano,
huku hatua stahiki zikichukuliwa.
0 comments:
Post a Comment