Venance Matinya, Mbeya
AGIZO la Rais John Magufuli kutaka
machinga wasibughudhiwe, limezua sintofahamu kwa viongozi wa halmashauri ya
Jiji la Mbeya, baada ya wafanyabiashara hao kutoka nje ya soko na kujenga mabanda
kwenye maeneo yasiyostahili.
Sintofahamu hiyo ilitokea juzi, baada ya
machinga hao wapatao 24 kuamua kujenga vibanda vya biashara nje ya Soko la
Sokomatola kinyume na taratibu, huku wakisisitiza kuwa wanafuata Kauli ya Rais
kwamba hata ikiwezekana wafunge hata barabara ili wafanye biashara zao.
Kutokana na hali hiyo, Uongozi wa
Halmashauri ya Jiji la Mbeya ulibomoa vibanda hivyo, hali iliyozua vurugu baina
ya mgambo wa Jiji na wafanyabiashara hao wakidai waachwe waendelee na biashara,
licha ya kukiri eneo hilo haliruhusiwi kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika kikao cha usuluhishi
ambacho kiliitishwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David
Mwashilindi na kuhudhuriwa na Mbunge wa Mbeya mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi,
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Zakaria Machoa alisema kwa mujibu wa sheria
wafanyabiashara wakihitaji eneo la biashara lazima waandike barua ambayo
itapita serikali ya Mtaa, Kata kisha Halmashauri.
Alisema wafanyabiashara hao walijiamulia
wenyewe bila kufuata taratibu za kuomba kupanua eneo la soko ili waweze kuuzia
nje ya Soko kwani hata Ofisi ya Serikali ya Mtaa haikuwa na taarifa wala Ofisi
za Kata, pia hazikuwahi kupokea barua za maombi kutoka kwa wafanyabiashara hao.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Soko la
Sokomatola, Abdalah Shaibu alikiri kuandika barua ya kuomba kupatiwa eneo,
lakini haikujibiwa hadi hapo wafanuabiashara walipoamua kuanza kujenga vibanda
ili wafanye biashara kutokana na ufinyu wa maeneo na kusisitiza kuwa uamuzi
waliochukua ni kuunga mkono kauli ya Rais Dk. Magufuli.
Aidha baadhi ya Wafanyabiashara
waliobomolewa vibanda vyao walikiri kufanya ujenzi huo kinyume cha taratibu
ambapo waliuomba uongozi wa Jiji kutumia busara kuwaruhusu kuendelea kufanya
biashara katika eneo hilo hadi utaratibu mwingine utakapotolewa.
“Nikuombe Mkurugenzi na Meya tumieni
Busara kama ilivyotumika katika masoko mengine kama Kabwe na Mwanjelwa
mturuhusu tufanye biashara kule ndani hakutoshi na sisi tupo tayari kulipa
ushuru na kufuata taratibu zote” alisema Beth David Mfanyabiashara Sokomatola.
Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi
(SUGU) alisema msimamo wake tangu 2010 ni kuona kila mwananchi anapewa haki ya
kujitafutia riziki hivyo anaungana na wafanyabiashara kumuomba Meya awaruhusu
kufanyabiashara eneo hilo kwa masharti ya kuzingatia usafi wa Jiji.
“Mimi kama Mbunge nabariki
Wafanyabiashara kuendelea na biashara katika eneo hili lakini tuzingatie usafi
na maboresho mengine ya kuhamisha au kutafuta eneo lingine tutafuata taratibu
za vikao hivyo naomba Mheshimiwa Meya waruhusu watafute riziki wananchi hawa”
alisisitiza Sugu.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya,
Mchungaji David Mwashilindi alisema Halmashauri ya Jiji limewaruhusu kufanya
biashara eneo hilo kwa muda hadi watakapotafutiwa eneo la kudumu kwani
kinachotakiwa ni Halmashauri kuwa na amani na utulivu.
Aliongeza kuwa wataendelea kuwepo hapo
hadi pale utaraibu wa kuwaondoa wafanyabiashara wote wanaofanya maeneo ambayo
hayaruhusiwi hususani barabarani kwa kuwatafutia maeneo ya kwenda kabla ya
kuwaondoa kabisa.
0 comments:
Post a Comment