Seif Mangwangi, Arusha
George Simbachawene |
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George
Simbachawene, amesema amewateua wajumbe wa bodi ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali
za Mitaa (LAPF) ili kufanya kazi ya wananchi na sio kupiga dili kupitia mfuko
huo.
Pia, amesema migogoro mingi ndani ya
mashirikia ya Serikali imekuwa ikichangiwa na wajumbe wa bodi kutaka kufanya
biashara na madalali na kusahau kazi zao kama waelekezi na wasimamizi wa
menejimenti.
Simbachawene aliyasema hayo jana jijini
hapa alipokuwa akizindua bodi ya wadhamini ya mfuko wa LAPF ambayo itafanyakazi
yake kwa miaka mitano huku akisisitiza uadilifu kwa wajumbe.
Aliwataka wajumbe kuendeleza mambo
mazuri yaliyofanywa na bodi iliyomaliza muda wake na kuwataka kuzalisha ajira
katika sekta ya viwanda ili kukuza ajira sanjari na kusimamia maslahi ya
wanachama kwa kuondoa malalamiko ikiwemo kulipa mafao yao kwa wakati.
"Ni vyema wajumbe wa bodi mkaepuka
migogoro kwa kufanya biashara za dili na madalali wa pembeni badala yake
msimamie rasilimali za mfuko huu kwa uadilifu na weledi kwa maslahi ya nchi na
wanachama wenu," alisema.
Alisema ni vyema mfuko huo ukaangalia
aina ya uwekezaji katika sekta ya viwanda utakaoibua ajira kwa vijana ikiwemo
kuondoa malalamiko baina ya wanachama na menejimenti ya LAPF.
"Bodi hii niliyoichagua ni bodi
yenye wasomi wengi na haina wanasiasa hapa, ukweli wa Mungu sijaagalia urafiki
wakati wa uteuzi, fanyeni kazi kwa weledi na kuepukana na dili ambazo
hazitaleta tija katika mfuko huu, menejimenti ni bodi mshirikiane katika
kuhakikisha mfuko huu unajivunia ile kauli mbinu ya kulipa jana hivyo
zingatieni ushauri mnaopewa na wataalam na fanyeni kazi hoja mbalimbali na
kisha kutoa maelezo," alisisitiza.
Aidha Waziri Simbachawene aliitaka bodi
hiyo kudhibiti gharama za uendeshaji wa mfuko na kujenga mahusiano mazuri kati
ya menejimenti na bodi kwaajili ya kuleta ufanisi nzuri wenye tija na
mafanikio.
Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Profesa
Faustine Bee ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha biashara cha Ushirika
Moshi, Kilimanjaro alimshukuru Rais John Magufuli kwa kumteua kuwa Mwenyekiti
wa bodi hiyo yenye jumla ya wajumbe saba wa Kada mbalimbali.
Wajumbe hao wengine ni pamoja na Dk
Rehema Kilonzo anayetokea chuo Kikuu cha Dodoma, Suleiman Kikingo, Henry
Kabatwa, Wakili Cornelius Kariwa pamoja na Tumaini Nyamhokya
Mkurugenzi wa mfuko huo, Eliud Sanga
alisema mfuko huo wa Lapf ni mfuko wa kipekee unaojali wanachama sambamba na
kupokea tuzo mara sita mfululizo ya utunzaji wa hesabu huku ikiwa na mikakati
ya kuinua sekta ya viwanda na kuzalisha ajira kwa watu mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment