Fidelis Butahe, Dodoma
HISA za Uda zawa kaa la moto. Ndivyo
unavyoweza kusema baada ya jana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni,
Freeman Mbowe kufanya kikao cha dharura na mameya, naibu mameya na viongozi
waandamizi wa Ukawa kujadili utata wa uuzwaji wa hisa za Shirika hilo la
Usafiri Dar es Salaam.
Mameya hao kutoka Dar es Salaam
waliwasili mjini hapa juzi kwa nyakati tofauti, kuhudhuria kikao hicho
kilichofanyika jana kwenye ofisi za Bunge.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
zilieleza kuwa kikao hicho kilifanyika baada ya kuibuka mvutano kati ya
Serikali na uongozi wa Jiji hilo, linaloongozwa na Ukawa kuhusu kuidhinisha Sh
bilioni 5.8 za uuzwaji wa hisa asilimia 51 kati ya 100 kwa kampuni ya Simon
Group.
Jumamosi iliyopita Baraza la Halmashauri
ya Jiji hilo chini ya Meya wake, Isaya Mwita kwenye kikao chake cha kawaida,
lilishindwa kufikia mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kwa kilichoelezwa
ni sawa na kubariki ufisadi wa uuzwaji wa hisa hizo ambazo wanaona ni kiasi
kidogo.
Kikao hicho kilifanyika baada ya agizo
la Rais John Magufuli Januari 27 wakati akizindua mradi wa mabasi yaendayo
haraka.
Katika agizo hilo, Rais alitoa siku tano
kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha kiasi hicho cha fedha zilizolipwa na Simon Group
kinapangiwa matumizi.
Lakini jana, Mbowe ambaye ni Mwenyekiti
wa Chadema aliliambia gazeti hili nje ya viwanja vya Bunge, kuwa amewaita
mameya hao na manaibu wao ili kuzungumzia sakata la hisa hizo.
“Nataka tupate msimamo wa pamoja ili
wakazi wa Dar es Salaam wanufaike na na Uda. Sioni sababu ya kuiua wala
kulichukia shirika hili,” alisema.
Miongoni mwa mameya walioonekana jana kwenye
viwanja vya Bunge ni Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye alikiri kuitwa
kuhudhuria kikao licha ya kusisitiza kuwa hajui ajenda.
Mapema jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hana la kusema juu ya kushindwa kugawanywa
kwa fedha hizo.
Alitaka viongozi hao wapewe muda ili
kumaliza tatizo hilo huku akisisitiza kwamba kwa kuwa siku zimepita, anasubiri
kauli ya Rais juu ya jambo hilo.
0 comments:
Post a Comment