Mwandishi Wetu
WAKULIMA wadogo
katika mikoa 10 wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kupata kuwezeshwa
kubadili mfumo wa maisha kupiti kilimo.
Katibu Mtendaji
wa Mfuko Kichochezi wa Kuendeleza Kilimo Biashara Ukanda wa Kusini mwa
Tanzania, Dk. John Kyaruzi alisema Dar es Salaam jana kuwa kuna fursa nyingi
kwa wakulima wadogo wanaojiunga katika vikundi.
Dk. Kyaruzi
alisema, ili kubadili mfumo wa kilimo na kuwa cha biashara lazima kuwepo na
mazao ya kutosha ambayo yana ubora, miundombinu mizuri ikiwemo barabara na
upatikanaji wa maji ya uhakika kwa mwaka mzima.
“Mkulima mdogo
ana changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa mtaji, mbolea, dawa za kuua wadudu
shambani, mbinu bora za kuhifadhi mazao kabla ya kuyauza, vifaa bora vya kisasa
pamoja na uhakika wa soko. Yote haya yapo chini ya uwezo wetu, tunachotaka
wakulima wajiunge na wapeleke malalamiko yao kwa kampuni au taasisi moja ambayo
tutaitumia kutatua matatizo yao.
Akitoa mfano alisema
wakulima wa miwa Morogoro au Kagera, wakilalamika ubovu wa barabara
watazungumza na Kiwanda cha Sukari Mtibwa au Kagera Sugar watengeneze hizo
barabara kisha wawape mchanganuo na kuwalipa, au wakulima wakilalamika ukosefu
wa pembejeo watazungumza na kampuni inayosambaza pembejeo itoe huduma hiyo kisha
wao ndio hulipa gharama zote.
“Tunachotaka ni
kumaliza changamoto zinazomfanya mkulima ashindwe kutoa mazao bora na mengi,
kwa kawaida soko linataka kitu kilicho bora kwa idadi kubwa. Kiwanda cha nyanya
kinaweza kuhitaji tani 1000 kwa siku, lakini wakulima katika mkoa husika uwezo
wao ni kulima nusu yake lazima mwekezaji ataagiza bidhaa hiyo nje ya nchi, sisi
tunataka kuondoa hilo,” alisema DK. Kyaruzi.
Akizungumzia
matatizo ya kukopesha wakulima alisema, huo si uamuzi sahihi kwa sababu kumkopesha
maana yake ni kumfunga mkulima asiwe huru kwa kile anachofanya akifikiria namna
ya kurudisha fedha alizokopa.
“Wakulima wadogo
wana matatizo mengi ya kifedha, mkopo hauwezi kuwa suluhisho la matatizo yao
zaidi ya kuongeza matatizo, unaweza kumpa mkopo mkulima akaanza kutatua
matatizo ya nyumbani ikiwemo afya au sare za shule za mtoto wake, hadi akianza
kulima fedha yote ameimaliza kwenye matatizo ya kifamilia, tukasema mbinu hii
si muafaka,” alisema Dk. Kyaruzi.
Kwa sasa mfuko
huo unasaidia wakulima katika mikoa 10 ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro,
Pwani, Dodoma, Singida, Rukwa, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya na Rukwa, ambapo mfuko
huo wa kuchochea kilimo unalenga ongezeko la viwanda maeneo hayo kulingana na
aina ya mazao yanayolimwa ikiwemo matunda, mbogamboga, nafaka na mifugo.
0 comments:
Post a Comment