Mwandishi Wetu, Serengeti
WASICHANA zaidi ya 4,000 wilayani hapa wameokolewa
dhidi ya ukeketwaji kwenye makabila ya Wakurya na Wangoreme.
Katibu Tawala wa Wilaya, Cosmas Qamara
alibainisha hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukeketaji katika Kituo
cha Nyumba Salama yenye kaulimbiu: Tujenge Ushirikiano Imara Kati ya Afrika na
Dunia kutokomeza ukeketaji kufikia mwaka 2030.
Qamara alisema katika msimu uliopita
wasichana 5,621 walikuwa wameandaliwa kukeketwa kati yao 4,100 sawa na asilimia
74 waliokolewa na 1,473 kukeketwa sawa na asilimia 26 ya walengwa.
Alisema mafanikio hayo yalitokana na mradi
wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti, unaotekelezwa na Amref Health Africa Tanzania,
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Washehabise, Shirika la Imara, Nyumba
Salama, Dawati la Jinsia la Polisi na wadau wengine chini ya ufadhili wa UN
WOMEN, mabadiliko katika jamii yalionekana.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuwachukulia
hatua kali za kisheria wote wanajihusisha na vitendo vya ukeketaji, hatuwezi
kuendekeza mambo yasiyo na msingi kwa maslahi ya mtu binafsi lazima tufike
mahali suala hili likomeshwe kabla ya mwaka 2030,’’ alisema Qamara.
Ofisa Mradi wa Tokomeza Ukeketaji
Serengeti, William Mtwazi alisema katika kipindi cha mwaka mmoja cha mradi wa
Tokomeza Ukeketaji waliokoa wasichana 241 na kuwapeleka Nyumba Salama kwa
usalama wa maisha yao.
Alisema watuhumiwa 32 wa makosa ya ukeketaji
walikamatwa na kesi zilizo mahakamani ni 10 huku tatu zikiwa tayari
zimehukumiwa na washitakiwa waliofungwa ni wanne.
‘’Katika siku hii maalumu ya kupinga
ukeketaji duniani, tunazitaka jamii zinazoendeleza ukeketaji, kuacha mara moja
kwa kuwa madhara yake ni makubwa kwa watoto wa kike na wanawake kwa jumla,’’ alisema
Mtwazi.
Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa
Wilaya, Alfred Kyebe alisema mikakati inahitajika kukomesha vitendo hivyo
ambavyo vinakumbatiwa na wazee wa kimila, mangariba na wazazi.
Alisema watoto wengi wanapofikishwa Polisi
huwa wameandaliwa kusema uongo kwa lengo la kunusuru watoto wao na huchangia
kuharibu ushahidi wa kesi nyingi.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi,
Christopher Genya alisema chanzo cha kukithiri ukeketaji ni mitizamo hasi ya
baadhi ya wazazi ambao wanaona ukeketaji una faida kimila na desturi.
Alisema umefika wakati wa kuachana na
ukeketaji na badala yake kusomesha watoto wa kike ili kujenga Taifa lenye usawa
ambalo linathamini utu wa mwanamke kabla ya mwaka 2030.
Baadhi ya watoto waliokimbia ukeketaji
walio Nyumba Salama waliiomba Serikali iwasaidie kupiga vita unyanyasaji wa
kijinsia na kuwachukulia hatua wanaojihusha na vitendo hivyo kwa kuwa ukeketaji
hauna faida.
0 comments:
Post a Comment