Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu
Kassim Majaliwa amesema kuanzia Machi mosi, Serikali itapiga marufuku matumizi
ya pakiti za plastiki kufungashia pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’.
“Tumekaa na
wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza pombe waziweke kwenye ukubwa
unaokubalika.
“Sasa hivi
viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu
ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia tarehe moja Machi,
tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye,” alionya.
Waziri Mkuu alitoa
kauli hiyo juzi jioni wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani,
wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.
Alisema agizo
hilo linakwenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya, kwani mji wa Mirerani
unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.
“Tutawakamata
wanaosambaza, wanaouza na wanaokula. Hapa Mirerani kuna bangi, kuna mirungi, kokeni
na heroin. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni kupambana na dawa za
kulevya. Piteni kwenye vijiwe na kukagua wanaolegealegea, kisha tuwapime,”
alisisitiza.
Akifafanua kuhusu
uwekezaji kwenye eneo la Shambalai kutokana na ujumbe ulioandikwa kwenye
mabango, Waziri Mkuu alisema katika eneo hilo zimetengwa ekari 500 kwa ajili ya
EPZA ili kujenga miundombinu.
“Hilo eneo ni la
uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, masoko na maduka makubwa. Sote
tunafahamu, kuwa Tanzania hivi sasa inaweka msisitizo juu ya ujenzi wa viwanda.
“Pale tunataka
tuwe na viwanda vya nyama, vya kushona nguo na kuchakata madini ya tanzanite
ili kuyaongeza thamani,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema kama
kuna mtu ana uhakika kuwa nyumba yake bado haijalipwa fidia eneo lile, akaonane
na Mkuu wa Mkoa, Dk Joel Bendera lakini taarifa alizopewa ni kwamba hakuna mtu
ambaye hajalipwa.
Waziri Mkuu pia
aliwaita wakurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne wampe taarifa ya malalamiko ya
wafanyakazi wa kampuni hiyo kwamba hali ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo
ikimilikiwa na Wazungu kuliko sasa.
“Nikimaliza
ziara ya mkoa huu, nataka Februari 27, wakuu wa hii kampuni waje ofisini kwangu
na taarifa kuhusu shughuli za uendeshaji wa madini. Nitawashirikisha wabunge
wenu ili waje waseme kwa nini Mzungu ni bora kuliko Mtanzania,” alisema.
“Serikali hii
inatarajia kuona Watanzania wakinufaika na rasilimali zao. Haiwezekani
tukahimiza uwekezaji wa ndani halafu leo anasifiwa Mzungu kuliko mzawa,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment