*Asema atafuata sheria, wanasheria wanena
Suleiman Msuya na Charles James
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Siyanga amesema mfumo uliotumika na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hivi karibuni kutaja majina ya
watuhumiwa wa dawa hizo ni tofauti na utaratibu wa utendaji kazi wa kamisheni
yake, akieleza watajikita katika kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na sheria.
Aidha, Siyanga amesema licha ya
kukabidhiwa majina 97 na mkuu huyo wa mkoa katika jalada lililosomeka, ‘majina
97 ya wauzaji dawa za kulevya wakubwa’ yeye atawachunguza watu hao na kufuata
taratibu zote za kisheria katika kuwachukulia hatua, lakini wanasheria wamesema
Makonda anaweza kusababisha Serikali kushtakiwa.
“Kutangaza majina si kipaumbele chetu
sisi tunazingatia uchunguzi na mahojiano ambayo yanaweza kutupatia taarifa
zaidi za wahusika kwani huu ni mtandao wa kidunia,”alisema.
Kauli hiyo ya Siyanga inaweza
kutafsiriwa kuwa ni kumkosoa Makonda kwa kutaja majina ya watu 65 akiwahusisha
na dawa za kulevya, jambo linalotajwa pia kuwa kinyume cha sheria.
Alisema kimsingi mapambano ya dawa za
kulevya yalikuwa yakitaribiwa wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na sheria
husika ilitoa nafasi pia kwa mamlaka mbalimbali kujihusisha na operesheni hiyo hadi
kufikisha watuhumiwa mahakani.
Kamishna huyo alisisitiza kuwa kwa
mujibu wa Sheria ya mwaka 2015 wanayoisimamia, kutaja majina si kipaumbele
kikuu kwao na kwamba wanazingatia uchunguzi zaidi ili kubaini mtandao mzima wa
dawa za kulevya.
Alisema kupambana na dawa za kelevya si
jambo rahisi na kuwa wanaohusika na biashara hiyo ni watu ambao kwenye jamii
wanaonekana wasafi hivyo ni vema kujipanga.
Alisema suala la watu wanaodaiwa kutumia
dawa za kulevya kufikishwa mahamakani limejikita katika pande mbili ambazo ni
baada ya mhusika kukataa kutumia, lakini pia inaweza kuwa ni sehemu sahihi ya
kumtaka mhusika kuacha na huwekwa katika uangalizi.
Siyanga alitoa wito kwa watumiaji wa
dawa za kulevya kutoa ushirikiano ili waweze kuwasaidia kwani ni moja ya
majukumu yao.
Kesi
ya Manji
Alipotakiwa kueleza ni kwa nini Manji
alipelekwa mahakamani alisema kimsingi kesi hiyo haiwahusu kwa sababu ilianza
kupitia mamlaka nyingine kabla ya mamlaka yake kuanza kazi.
Mapapa
wa dawa za kulevya
Kwa upande mwingine, Siyanga alisema
mamlaka yake inatarajia kuzunguka katika magereza mbalimbali duniani na
kuzungumza na Watanzania ambao wamehukumiwa kunyongwa na vifungo vya maisha ili
waweze kuwataja watu ambao wanawatuma kufanya biashara hiyo.
Alisema kupitia utaratibu huo wanaweza
kukabiliana na tatizo hilo huku akibainisha kuwa akitolea mfano mfanyabiashara
mkubwa ambaye ni mwanamke amehukumiwa kifungo jela, baada ya wafungwa zaidi ya 40
nchini Ujerumani, kubainisha kuwa yeye ndiye aliwatuma.
Kamishna Siyanga alisema pia
mfanyabiashara mwingine mkubwa mwanaume, amehukumiwa kwenda jela mwaka 2010
baada ya kubaini mtandao mzima wa tatizo hilo na kuwa mkakati wao ni kumaliza
mtandao zaidi.
“Huyu mwanamke yupo gerezani kati ya
Segerea au Keko. Huyu mwanaume pia yupo katika magereza yetu,”alisema.
Alisema Tanzania imekuwa ikikamata hadi
tani 1.5, kilo 800, 200, 100, 50 hivyo wapo katika mapamano ya kuhakikisha kuwa
hali hii inakabiliwa.
Wanasheria
wanena
Wakati Siyanga akieleza hayo, wanasheria
wameeleza kwa kuandika ‘majina 97 ya wauzaji wa dawa za kulevya wakubwa,
Makonda anaweza kusababisha Serikali kushtakiwa wakisema inawezekana hakuwa
anajua anachokifanya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanasheria
hao walisema kilichofanywa na Makonda kuandika watu hao ni wauzaji, kisheria ni
kosa kwani tayari alikuwa amewahukumu wakati yeye hana mamlaka hayo.
“Sijui alitoa wapi uwezo wa kuandika
kwamba hao watu 97 ni wauzaji wakati bado hata hawajapelekwa mahakamani,
achilia mbali kukamatwa. Nafikiri hakuwa anajua nini anakifanya ile kwenye
sheria ndiyo tunaita ‘defamation’ yaani unampa mtu hukumu hata kabla ya
kumfikisha Mahakamani:
“Hakuna mahali popote kwenye Katiba ya
Tanzania inayompa mtu mamlaka hata Rais ya kumhukumu mtu tofauti na mahakama,
hiki ndio chombo kinachoweza kusikiliza kesi, kuitolea ufafanuzi na kutoa
hukumu tofauti na hapo unaweza baadaye kushtakiwa kwa kuchafua majina ya watu,”alisema
Joseph Kiwanga wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kauli hiyo iliungwa mkono na Wakili
James Marenga ambaye alisema sheria ipo wazi kuwa chombo pekee chenye uwezo wa
kuhukumu nchini ni Mahakama na siyo Bunge, Baraza la Wawakilishi wala Serikali
Kuu.
“Kilichofanywa na Makonda ni kinyume na
sheria na endapo watu hao wakihojiwa na kukosekana na hatia wanaweza kufungua
kesi ya madai. Katiba yetu inasema vizuri kabisa katika ibara ya 107 A kifungu
kidogo cha kwanza kwamba mahakama ndio yenye mamlaka kisheria ya kusikiliza kesi
na kumtia mtu hatiani au baada ya kumkosa na hatia hapo mtu huyo anakuwa hana kosa
lolote lililothibitika.
“Sheria ilivyo hata kama polisi
wamekamata kundi la mateja wanaotumia dawa za kulevya, au wamefanikiwa
kuyakamata majambazi bado hawawezi kukupeleka moja kwa moja Segerea au Ukonga
japo wana ushahidi hadi upelekwe mahakamani, upelelezi ufanyike ndio mahakama
iseme kama imemkuta na hatia, tofauti na hapo unatuhumiwa tu,”alisema Marenga.
Wakili Marenga alisema kifungu cha 13
cha Katiba kinatoa haki ya mtuhumiwa kusikilizwa kwanza kabla ya kuhukumiwa na
kuongeza kuwa kama watu hao hawatokutwa na hatia wanaweza kuidai fidia Serikali,
jambo ambalo linaweza kulisabishia hasara Taifa kwa kulipa kundi kubwa la watu.
Kwa upande wake Mhadhiri wa UDSM, Dk James
Jesse alisema kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa ni makosa kwani alihukumu kabla ya
kuwapeleka mahakamani na kwamba kama hana ushahidi wa kutosha dhidi ya watu hao
ni rahisi kufunguliwa kesi ya kuchafua majina yao.
Hata hivyo, upande wake Wakili Ufforo
Mangesho kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema inawezekana
Makonda alikuwa na lengo tofauti na ndiyo sababu ya kuyaita majina hayo
‘wauzaji’ badala ya watuhumiwa huku akijua hana uhalali wa kisheria wa
kumhukumu mtu.
“Inawezekana kulikuwepo na kingine nyuma
ya vita ya dawa za kulevya kwa sababu ninachoamini Makonda alikuwa anajua
kabisa kwamba anavunja sheria kwa kuhukumu majina ya watu hadharani ilihali
mahakama zipo na ndio zenye wajibu kikatiba wa kushughulikia kesi na kutoa
hukumu,”alisema Mangesho.
Februari 13, Mwaka huu wakati akitangaza
awamu ya pili ya kile anachokiita vita dhidi ya dawa za kulevya Mkuu huyo wa
Mkoa alimkabidhi jalada hilo kamishna Sianga huku likiwa limeandikwa kwamba ni
majina ya ‘wauzaji ’ wa mihadarati hiyo jambo ambalo lilileta tafsiri tofauti
miongoni mwa wanasheria wakihoji uhalali wa Makonda kuhukumu.
0 comments:
Post a Comment