Hussein Ndubikile
Mwanamema Shein
|
MKE
wa Rais wa Zanzibar, Mwanamema Shein, amesema vitendo vya udhalilishaji wa
kijinsia kwa wanawake na watoto vimekuwa sugu katika jamii kwani vinasikika
kila siku lakini havijapata ufumbuzi.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa Ikulu ya Zanzibar, Mwanamwema alitoa kauli hiyo
jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani wakati akifungua kongamano
la siku moja liliozungumzia udhalilishaji.
Kongamano
hilo liliandaliwa na Taasisi ya Mwanaharakati, Bibi Siti Bint Saad.
Alisema
licha ya kuwepo kwa kampeni dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa
kijinsia iliyoanzishwa mwaka 2014, bado jamii ina wajibu wa kutafuta mbinu na
mikakati zaidi hasa ya kuelimisha ubaya wa vitendo hivyo.
“Tuna wajibu wa kuchukua hatua za haraka kwani wahenga walisema ‘usipoziba ufa, utajenga ukuta’, sote tuache muhali,
tuchukue hatua ili tuepuke kujenga ukuta kwani ni dhahiri vitendo vya udhalilishaji haviwezi kutusaidia
kuwa na jamii bora ya waungwana na wastaarabu wenye maadili mema,” alisema.
Aliitaka
jamii kulinda haki za watoto na kuwakinga na vitendo vya udhalilishaji kwa
kuziimarisha familia kwani familia zisizo imara huvunjika na kusababisha
matatizo kwa watoto hasa kukosa malezi bora na haki zao nyingine.
Aliipongeza
taasisi hiyo na nyingine kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Saba
katika kukabiliana na vitendo hivyo vibaya.
Mke
wa Rais alisisitiza kuwa baadhi ya tafiti zilizofanywa hivi karibuni zinaonesha
idadi ya talaka imeongezeka katika jamii sababu ambayo inatajwa kusababisha
watoto kukosa ulinzi na watu wabaya kupata nafasi ya kuwadhalilisha.
Aliwataka
wanandoa kuendelea kustahamiliana na kuwataka wazee wazidi kuzilinda ndoa za
vijana wao kwa kuwasisitiza umuhimu wa kuvumiliana na kusameheana ili wajukuu
wapate malezi bora.
Mwanamwema
aliwasihi pia viongozi wa dini kuelimisha ubaya na athari za talaka.
Aliisisitiza
kuwa katika kukabiliana na vitendo hivyo ni lazima wazazi wawe mstari wa mbele kuhakikisha
watoto wanapata haki zao ikiwemo elimu huku akisisikitishwa kusikia kuwa katika
jamii bado kuna wazazi wanaowakatisha masomo watoto wao ili waolewe.
Aliunga
mkono kaulimbiu ya kongamano hilo inayosema kwamba; “Kina Mama Tumesema Unyanyasaji
wa Kijinsia Sasa Sasi”.
Kwa
upande wake, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto,
Maudline Cyrus Castico alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi
zinazopiga vita vitendo hivyo inatekeleza wajibu wake kwa ushirikiano mkubwa
na taasisi hizo zikiwemo za Serikali na zisizo za kiserikali.
Alifafanua
kuwa Serikali inayoongozwa Dk. Shein haitakaa kimya ili kuhakikisha inatokomeza
vitendo hivyo na mikakati mbalimbali imewekwa kufikia azma ya malengo
yaliyowekwa na kueleza kuwa vitendo hivyo vilikuwepo tangu zamani lakini
vilikuwa havitolewi taarifa.
Mwenyekiti
wa taasisi hiyo, Nasra Mohammed Hilal alielezea umuhimu wa kushirikiana katika
kupiga vita vitendo hivyo na kusisitiza kuwa kongamano hilo ni kati ya maagizo
na maazimio ya taasisi yake.
0 comments:
Post a Comment