Ahmed Makongo, Bunda
BAADHI ya walimu katika shule za msingi kwenye
Halmashauri ya Mji wa Bunda, mkoani Mara, wamekimbia vituo vyao vya kazi wakati
wa mchakato wa uhakiki wa vyeti na kushindwa kuhakikiwa.
Kufuatia hali hiyo, walimu wakuu wa
shule ambazo walimu hao walitoroka, wametakiwa kuandika majina na taarifa
sahihi juu ya walimu hao ili waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Hayo yalielezwa juzi na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Bunda, Janeth Peter Mayanja wakati wa kikao cha kazi
kilichoitishwa na uongozi wa halmashauri hiyo kwa ajili ya kuwapongeza walimu
wa shule kumi za msingi zilizofanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba
mwaka jana.
Mayanja alisema kuwa kuna baadhi ya
walimu wa shule za msingi katika halmashauri ya mji huo wakati wa uhakiki wa
vyeti, walitoroka kwenye vituo vyao vya kazi na kushindwa kuhakikikiwa na
kwamba walimu hao wasidhani kwamba uhakiki umeisha.
“Hiyo taarifa mnayo mnaijua kwamba
baadhi yenu wakati wa uhakiki wa vyeti walitoroka na sasa wamekwisharejea
wanadhani kwamba uhakiki umekwisha,” alisema Mayanja.
Alisema kuwa walimu wakuu wa shule hizo sasa
wanapaswa kuandika taarifa sahihi juu ya walimu waliokuwa wametoroka na sasa
wamerejea na kwamba mwalimu mkuu atakayetoa taarifa za uongo atatumbuliwa yeye
mwenyewe.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji huo,
Mayaya Magesse aliwataka walimu kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi wa
umma, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati sahihi.
Afisa Elimu Taaluma kwa Shule za Msingi
katika halmashauri hiyo, Reuben Kaswamila alisema kuwa kikao hicho ni cha kazi
kwa ajili ya kuboresha elimu.
Baadhi ya walimu ambao shule zao
zimefanya vizuri walisema kuwa hali hiyo imetokana na ushirikiano mzuri wa
walimu, wanafunzi pamoja na wazazi.
Shule ambazo zilipongezwa ni Olympus,
Day Star, ST. Paul na Muzuma, pamoja na shule za serikali za Kabarimu B,
Bukore, Bigutu, Kung’ombe A, Kabarimu A na Bitaraguru B.
0 comments:
Post a Comment