Suleiman Msuya
James Mbatia |
BARAZA la wadhamini la chama cha
NCCR-Mageuzi, limewataka wanachama na wapenzi wa chama hicho, kupuuza taarifa
zinazosambazwa mitandao, zikimhusisha Mwenyekiti wao James Mbatia,
kujimilikisha mali za chama.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mohammed
Tibanyandera, alitoa kauli hiyo jana katika taarifa yake iliyotolewa kwenye
vyombo vya habari.
Kauli hiyo ya Tibanyendera imetolewa
siku moja baada ya kada wa chama hicho, Faustine Sungura, kujitokeza katika
vyombo vya habari na kutangaza kusudio la kumfikisha mahakamani Mbatia na
Katibu Juju Danda, akiwatuhumu kuuza na kujimilikisha mali za chama kinyume na
taratibu.
Tibanyendera alisema tuhuma hizo si za
kweli na kwamba wanazozisambaza, wana mpango maalumu ambao wadhamini hawawezi
kuuvumilia.
Alisema NCCR-Mageuzi ni chama kinachofanya
uamuzi kupitia vikao vilivyoainishwa kikanuni na habari hizo hazina baraka za
vikao halali vya chama.
Kwa mujibu wa Tibanyendera, Katiba ya
chama hicho ya mwaka 1992 toleo la saba la mwaka 2014, imeagiza usimamizi wa
mali za chama kuwa chini ya uangalizi wa Baraza la Wadhamini, kama ilivyotamkwa
katika ibara 26 (7) (a) na (b).
“Tunapenda umma wa Watanzania na
wanachama wote, watambue kuwa Mwenyekiti au kiongozi yoyote asiyekuwa mjumbe wa
Baraza, hana mamlaka wala hawezi kuuza au kubatilisha umiliki wa mali za chama,
bila ridhaa ya Baraza la Wadhamini,” alisema.
Kuhusu mali zinazoondosheka, alisema
haziwezi kuwa mali za chama bila kuwepo kwa mikataba halali, inayosainiwa na mnunuzi
na muuzaji.
Alisema uuzwaji wa mali zinazohamishika,
hufanywa na Bodi ya Wadhamini kwa mujibu wa sheria inayosimamia muunganisho ya
wadhamini kifungu 318 ya mwaka 2002.
“Baraza lina uhakika kuwa hakuna mali
yoyote iliyotwaliwa binafsi inayomhusu Mwenyekiti, ingawa ana haki ya kumiliki,
kununua au kumiliki mali iwapo aliyoipata kihalali,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema hakuna
mwanachama yoyote aliyewahi kuwasilisha uthibitisho au kielelezo chochote cha
uwepo au umiliki wa shamba, kiwanja kilichouzwa au kumilikiwa na Mbatia.
Katika tuhuma za Sungura, alitaka chama
kitoe tamko rasmi kuhusu mali mbalimbali za chama, ikiwemo nyumba mbili katika
eneo la Bunju B wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, pamoja na shamba la
ekari 54 katika kijiji cha Kiromo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
“Barua zangu za Novemba 30, 2016 na Desemba
06, 2016 kwa Katibu Mkuu, zilizonakiliwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini
la NCCR – Mageuzi na ambazo hazikujibiwa, nakala zake zimeambatanishwa.
Ninaomba kurasa zake zipitiwe kwa umakini tafadhali,” alisema.
Sungura alidai baada ya kuchukua hatua
hiyo, mmoja wa viongozi wa karibu na Mwenyekiti, alimtumia ujumbe wa simu akimwambia
kuwa anaota ndoto, anapotea, ataharibikiwa, ana njaa, hana akili, aache roho
mbaya kuangalia mali za watu kwa husuda na ana familia inayomtegemea.
Kada huyo aliomba uuzwaji wa nyumba ya
vyumba 11 wilayani Tarime (Mara), nyumba ya vyumba sita Sumbawanga mjini
(Rukwa) na nyumba ya vyumba vitatu Mpanda (Katavi), usitishwe hadi tamko la juu
litolewe.
Alisema ni vema wanachama na wananchi
wakaelewa ukweli, kwani juhudi zake za kufatilia mali za chama kiofisi (kwa
kuandika barua), zimeshindikana badala ya kujibiwa kiofisi na baadhi ya
viongozi walio karibu na Mbatia wanatumia nguvu kuchafua jina lake.
“Ikibainika kama ninasema uongo, niko
tayari kuwajibika (kufukuzwa uanachama) kama ambavyo uongozi wako unavyotakiwa
kutoa kauli juu ya chama kumiliki mali hizo au la,” alisema.
JAMBOLEO lilifanikiwa kumpata Katibu wa
chama hicho, Danda ambaye alisema kinachofanywa na Sungura ni utovu wa nidhamu
kwa kile alichodai kuwa anajua taratibu zinazohitajika kufuatwa kwa hilo
analolidai.
“Kimsingi barua yake sijaipata, ila
namuomba afuate taratibu kwani anajua njia za kufuata na amekuwa katika chama
kwa muda mrefu, awe muwazi kuwa nataka nini ndani ya chama,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 26 Ibara
ndogo ya (2) ya Katiba ya chama hicho, mali za chama zinasimamiwa na wadhamini
hivyo ni vema akauliza hayo anayouliza.
0 comments:
Post a Comment