Leonce Zimbandu
Cassian Chibogoyo |
OFISI ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali imetoa
siku 44 kwa wachapishaji nchini kujiorodhesha kwenye ofisi hiyo kabla ya operesheni
ya kuwasaka nyumba kwa nyumba kuanza.
Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian
Chibogoyo, alisema Dar es Salaam jana, kwamba lengo la kuwataka kujiorodhesha ni
kuiwezesha Serikali na umma kuwatambua na kujiepusha kujificha iwapo
wanatekeleza wajibu wao wa uchapishaji kwa kuzingatia sheria.
Chibogoyo alikuwa akitoa msisitizo wa matumizi
sahihi ya vielelezo vya Taifa ambavyo ni Bendera, Nembo na Wimbo wa Taifa.
Alisema katika kuhakikisha suala hilo linafanikiwa,
Serikali imeandaa mkakati wa kukabiliana na wachapishaji wa nyaraka bandia hata
kama limefanikiwa lakini bado baadhi wanaendelea kukaidi.
“Unajua nyaraka bandia ni janga kwa
jamii, hivyo ofisi yangu inawataka wachapishaji kujiorodhesha hadi Machi 30, baadaye
tutafuata njia iliyotumiwa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kuhakiki vyeti, nasi
tutahakiki wachapishaji na ofisi za Serikali ambazo zimegoma kutundika Bendera
ya Taifa nchini,” alisema.
Alisema uchapishaji ni mwito tena una
maadili yake, hivyo ni lazima kuzingatia iwapo mchapishaji hawezi kufuata
taratibu zilizopo ni busara kutafuta biashara nyingine.
Aidha, Chibogoyo aliwataka vijana
wanaokimbiza Mwenge watoe maelezo kuhusu umuhimu wa Mwenge wa Uhuru hasa wakati
wa kuzindua miradi nchini.
Alisema maelezo hayo yatasaidia kuondoa
sintofahamu kwa watu ambao wanajenga hoja kuwa Mwenge hutumia pesa nyingi bila
sababu za msingi.
Alisema ikikumbukwe kuwa Mwenge wa Uhuru
ni miongoni mwa nyenzo za kuleta maendeleo ya nchi baada ya kuondoa maadui ujinga,
maradhi na umasikini.
Aliongeza kuwa baada ya Mwenge kuwekwa Mlima
Kilimanjaro, Watanganyika walijikusanya, kuungana na kupigania haki zao kwa lengo
la kujikomboa.
0 comments:
Post a Comment