*Ataja mambo 5 atakayopambana nayo
Suleiman Msuya
Mwigulu Nchemba |
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba, ametaja mambo matano makubwa, ikiwemo dawa za kulevya akisema wizara
yake haina mjadala na suala hilo kwani linagusa maisha ya Watanzania wote.
Nchemba alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam baada ya kushuhudia
viongozi mbalimbali wakiapishwa na Rais John Magufuli.
Walioapishwa ni pamoja na Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia
na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga.
Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini
Algeria, Omar Yusuph Mzee, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Joseph Sokoine
na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgovano.
Waziri Mwigulu alitaja mambo mengine ni
kupambana na ugaidi, ujangili wa rasimali za nchi, uhalifu wa kutumia silaha na
ubakaji.
Alisema wamejipanga kukabiliana mambo
hayo kutokana na ukweli kuwa yamekuwa yakiongezeka kila kukicha hali ambayo
inahatarisha amani ya nchi.
Mwigulu alisema wizara yake kwa sasa
imekamilika kila idara hivyo ni wakati mwafaka wa kuhakikisha mapambano yote yanayohusika
na mambo hayo matano yanafanikiwa.
Alisema dawa za kulevya ni janga linalohitaji
ushirikiano wa kada zote hivyo wao wapo tayari kuhakikisha vita hiyo
inakabiliwa kwa njia yoyote.
Waziri huyo alisema kwa siku za karibuni
kumekuwepo na matukio ya ubakaji na ujangili hasa nyara za Serikali akisema
waanamini kwa pamoja wataweza kupambana na wahusika.
“Tumejipanga kwa mambo makubwa matano
ambayo ni dawa za kulevya, ujangili, ubakaji, uhalifu wa kutumia silaha na
ugaidi ambapo vyote kwa pamoja vinashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu,”
alisema.
Alitoa mwito kwa Watanzania kutoa
ushirikiano wa mapambano mbalimbali ambayo yanafanywa na Serikali ili kudumisha
amani ya nchi.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia
madarakani imekuwa katika mkakati wa kupambana na matukio mbalimbali ya uhalifu
ambapo kwa siku za karibuni mapambano hayo yameonekana kushika kasi hususan
kwenye dawa za kulevya ambayo yalianzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda.
0 comments:
Post a Comment