Fidelis Butahe, Dodoma
Zitto Kabwe |
KITENDO cha Jeshi la Polisi kutaka kumkamata Mbunge wa
Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, juzi baada ya kutoka bungeni,
kilimfanya mbunge huyo kuondoka bungeni usiku wa manane kuamkia jana kwa msaada
wa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Juzi, wakati Zitto akiwasilisha hoja bungeni kuhusu
utaratibu wa wabunge, hasa wa upinzani kukamatwa na polisi bila utaratibu,
alibainisha kuwa hata yeye amepewa taarifa kuwa akitoka nje ya viwanja vya Bunge
atakamatwa, kuahidi kulala bungeni ili kuwakwepa polisi.
Baada ya wabunge wa upinzani kususia kikao cha Bunge juzi
saa 10:30 jioni kutokana na hoja hiyo kupingwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Zitto aliendelea kuwepo ndan ya eneo la Bunge hadi jana saa 6:25
usiku alipoondoka kwa msaada wa Ndugai aliyempatia usafiri.
Hata hivyo, kususia kikao kwa wabunge hao wa upinzani
sambamba na Zitto kusakwa na polisi, jana asubuhi kulimfanya Mwenyekiti wa
Bunge, Andrew Chenge kutaka Serikali na Bunge kufanya kazi kwa pamoja, huku
akisema taarifa ya kukamatwa hovyo kwa wabunge ataifikisha kwa Ndugai aliyedai kuwa ataitolea tamko rasmi leo.
Zitto asimulia
“Niliondoka saa 6 usiku ikiwa ni baada ya mashauriano
kati yangu na Katibu wa Bunge (Dk Thomas Kashilillah) na Spika Ndugai ambaye aliwasiliana na IGP (Mkuu wa Jeshi la
Polisi-Ernest Mangu),” alisema Zitto.
“Nilivyokuwa nawasilisha hoja yangu bungeni nilikuwa
najua kila kitu juu ya kukamatwa kwangu ndio maana nikaamua kutotoka bungeni
kwani walikuwa wakinisubiri nje ya viwanja wa bunge.”
Alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu, IGP
aliwasiliana na Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa ambaye
alibainisha kuwa mbunge huyo alikuwa akitafutwa kwa kutoa kauli uchochezi
alipokuwa mkoani Shinyanga, kubainisha kuwa polisi ilikiri kutoona kosa lake.
Alisema baada ya mashauriano hayo alihakikishiwa kuwa
akitoa hatokamatwa na polisi lakini kwa kujihami zaidi Spika Ndugai alituma
usafiri wa kumchukua.
“Spika aliwasiliana na mkuu wa ulinzi wa Bunge ili
kuniwezesha kutoka salama ila pamoja na kuwasiliana naye bado alinitumia gari
ambalo lilinitoa ndani ya viwanja vya Bunge,” alisema.
Juzi mpaka saa tatu baadhi ya mageti ya kutoka na
kuingilia ndani ya Bunge kulikuwa na magari ya polisi huku ulinzi ukiwa
umeimarishwa kwa kiwango kikubwa.
Kauli ya Mwenyekiti wa Bunge
Jana wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Tarime
Vijijini(Chadema), John Heche kuhusu polisi kuwakamata wabunge bila utaratibu,
Chenge alisema polisi wanaweza wasiwakamate wabunge pindi vikao vya Bunge
vinapokuwa vikiendelea, badala yake kufanya hivyo wakati mwingine.
Katika maelezo yake, Chenge alisema kuna haja pia ya
kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na Bunge kwa kuwa mihimili hiyo ina
majukumu yanayofanana.
“Heche nimekusikia ingawa hukueleza kwa undani, lakini
najua suala hili lilianza jana na Naibu Spika akalitolea ufafanuzi,” alisema.
“Ushauri wangu katika hili, kuna haja ya kuwa na
mahusiano mazuri kati ya Bunge na Serikali, lakini pia nakuomba Heche
umwandikie Katibu wa Bunge umweleze mapendekezo yako ili yafikishwe katika
Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa mjadala zaidi.
Alisema baada yah apo uongozi wa Bunge unaweza kujadiliana
na Serikali kwa sababu kama polisi wanamhitaji mbunge, wanaweza kusema wa
wakamkamata wakati mwingine kwa sababu wanajua anapoishi.
Awali, Heche alisema kama Bunge halitachukua hatua pindi
wabunge wanapodharirishwa, utafika wakati Bunge litaanza kudharirishwa.
Alisema Bunge ni chombo kinachoheshimika duniani kwa
sababu kinatunga sheria na kupitisha bajeti ya Serikali lakini hivi sasa
heshima yake.
“Hii tabia ya wabunge kukamatwa ovyo, tena bila
taarifa ya Spika, haipendezi na hata wakuu wa wilaya wanawanyanyasa sana
wabunge huko majimboni. Kwa hiyo, naomba mwongozo wako mheshimiwa mwenyekiti
ili uniruhusu niwasilishe hoja yangu ili Bunge liijadili,” alisema Heche.
Wabunge walivyotoka bungeni
Juzi, wabunge wa upinzani, walitoka nje ya Bunge wakionyesha
kutoridhishwa na majibu ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, aliyoyatoa wakati
alipokuwa akijibu taarifa ya kukamatwa kwa wabunge wa upinzani iliyowasilishwa
na Zitto.
Katika taarifa hiyo, Zitto aliwataja wabunge wa Chadema,
Godbless Lema wa Arusha Mjini aliyeko mahabusu katika Gereza la Kisongo, Arusha
kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali
anayetumikia kifungo cha miezi sita katika Gereza la Ukonga Dar es Salaam na
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi,
Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, wakati Dk. Tulia akijibu taarifa hiyo,
alisema kanuni za Bunge zinataka Spika wa Bunge apewe taarifa za kukamatwa
mbunge aliyetenda makosa ya madai na kama siyo makosa ya madai, hakuna haja ya
spika kupewa taarifa.
0 comments:
Post a Comment