Mwandishi Wetu
Dk. Hassan Abbas |
MAOFISA habari na mawasiliano serikalini, katika mikoa na halmashauri
nchini, wametakiwa kutumia njia za haraka na za kisasa katika mawasiliano,
ikiwemo matumizi ya tovuti na mitandao ya kijamii, ili kutangaza mafanikio ya
sera na mipango ya Serikali kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas,
alisema hayo jana jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa tovuti za halmashauri 35
za mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara,
Shinyanga na Simiyu.
Dk. Abbas alisema pamoja na kuwepo kwa vyombo mbalimbali vya habari vinavyotumika kufikisha taarifa za habari kwa wananchi, ikiwemo magazeti na redio, bado mitandao ya kijamii na barua pepe imendelea kutumiwa na watu wengi zaidi ulimwenguni kwa sasa.
“Kwa sasa nusu ya watu duniani wapo mtandaoni na hapa nchini kwa
mujibu wa ripoti ya TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano), Watanzania zaidi ya milioni
19 wapo mtandaoni aidha kwa kutumia barua pepe au kutembelea kurasa za Facebook,”
alisema Dk. Abbas.
Dk. Abbas alisema sifa za ofisa habari na mawasiliano wa karne ya
sasa, ni mwenye uwezo wa kutumia njia za kisasa za mawasiliano, zitakazomwezesha
kujibu hoja mbalimbali kwa haraka zaidi, badala ya kusubiri Serikali
kulalamikiwa na wananchi.
Alisema uzinduzi wa tovuti katika mikoa na halmshauri hizo, ni kigezo muhimu kitakachotumiwa na Serikali, kupima utendaji kazi wa maofisa habari katika kushughulikia kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Akifafanua zaidi, Dk. Abbas alisema lengo la Serikali ni
kuhakikisha tovuti za mikoa na halmashauri za wilaya nchini, zinaendelea kuwa
hai na zenye taarifa zilizozingatia muda na wakati na hilo litawezekana iwapo maofisa
habari watatimiza malengo wanayopaswa kujiwekea katika maeneo yao ya kazi.
“Litakuwa si jambo jema kuona baada ya miaka mitano, tovuti hizi zimesimama. Hii haitapendeza sana, hatuna budi kutambua kuwa Serikali na wafadhili wamewekeza fedha katika mradi huu, hivyo ni wajibu tukatimize wajibu wetu,” alisema Dk. Abbas.
Mkurugenzi wa Mji wa Magu, Fundikira Fundikira alisema Serikali inatambua changamoto zinazowakabili maofisa habari ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi na kutaka suala hilo lisitumike kama kigezo cha kuwakosesha wananchi taarifa.
“Sisi katika mkoa
tutahakikisha tovuti hizi zinasimamiwa na kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi
wetu. Tutahakikisha kuwa fedha za Serikali na wafadhili zinaleta tija kwa
wananchi wetu,” alisema Fundikira.
Mkurugenzi wa Miundombinu katika Wakala ya Serikali Mtandao (EGA),
Benjamin Dotto, alisema maofisa habari na Tehama, wanapaswa kuweka taarifa mpya
zilizozingatia muda kwa kuwa upatikanaji wake ni utekelezaji wa haki ya msingi
ya binadamum, pamoja na utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa
iliyosainiwa Serikali.
0 comments:
Post a Comment