Mashaka Mgeta
Profesa Anna Tibaijuka |
MIONGONI mwa walioguswa na tukio la Rais John Magufuli
kumsikiliza mjane, Swahaba Shosi, aliposhiriki kuhutubia Siku ya Sheria Februari
2, mwaka huu jijini Dar es Salaam ni Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna
Tibaijuka.
Rais Magufuli, baada ya kuhutubia hadhira iliyoandaliwa na
kuwashirikisha majaji, akajitokeza Shosi akielezea kuchoshwa na namna watendaji
wasiokuwa waadilifu katika taasisi tofauti za umma ikiwamo Mahakama,
wanavyopanga kumdhulumu haki ya kurithi mali za marehemu mume wake.
Baada ya kumsikiliza akijieleza kwa ujasiri, licha ya
majonzi yaliyomsababisha kutoa machozi takribani wakati wote alipojieleza, Rais
Magufuli aliamuru suala hilo lishughulikiwe haraka huku Shosi akipewa ulinzi na
jeshi la polisi.
Tukio hilo liligusa hisia za watu kwa namna tofauti,
wengi wao kupitia mijadala kwenye mitandao ya kijamii, wakimpongeza Rais Magufuli
kwa hatua hiyo.
Katikati ya hali hiyo, anajitokeza Profesa Tibaijuka, akisema
kadhia inayomkabili Shosi ni sawa na ile aliyokutana nayo, ikihusu ardhi
iliyoachwa na marehemu mume wake, lakini ikageuzwa na kufanywa hila aonekane
kuwa ni mporaji.
Lakini Tibaijuka kupitia waraka wake anasema, ni Rais
Magufuli alipofanya ziara mkoani Kagera hivi karibuni, kulitolewa taarifa za
uongozi dhidi yake (Profesa Tibaijuka) ambazo hata hivyo, mwitikio wake (Rais
Magufuli) ukawa mwenye kumsaidia dhidi ya wabaya wake.
Waraka wa Profesa Tibaijuka uliandikwa hivi:- Wanawake
hatuna budi kumshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kututetea sisi wajane tunaonyanyaswa
na mifumo dume na kuporwa haki zetu na watoto wetu.
Jana (Februari 2, mwaka huu) Rais alitenda makuu kuagiza
kwamba yule mama aliyekuwa ameonewa na kuhangaishwa kwa muda mrefu, sio tu kesi
yake isikilizwe lakini pia apewe ulinzi wa polisi.
Kwa kumbukumbu zangu, hii haijawahi kutokea kwa mnyonge
aliyekata kamba za ulinzi mkali unaomzunguka Rais badala ya kwenda rumande,
kupewa ulinzi wa polisi yeye mwenyewe. Hili linathibitisha kauli ya mara kwa
mara ya Rais Magufuli kwamba “msema kweli ni mpenzi wa Mungu”.
Kwa kuwa Rais Magufuli kajitanabaisha na kuudhihirishia
umma kuwa anachotaka ni ukweli na uwazi, huyu mama mwenzetu alikuwa na nguvu na
imani kwamba akimfikia (Rais Magufuli), matatizo yake yatakwisha.
Atapata kusikilizwa na haki yake ambayo vyombo vya
utawala na Mahakama vimeshindwa kumpatia kwa muda mrefu itapatikana. Vyombo
hivi hushindwa kwa sababu baadhi ya wahusika wanakuwa na maslahi binafsi katika
migogoro kama hiyo.
Wanaichukulia migogoro hiyo kuwa fursa na mtaji wasiopenda
uishe. Kwa hiyo anayedai haki yake anawekewa vikwazo na wale waliotarajiwa
kumsaidia.Kilio cha yule mama na maelezo yake yalikuwa wazi, kahangaishwa kwa
muda mrefu. Alikuwa tayari kujilipua. Ninampongeza mama kwa kutokata tamaa.
Na ninampongeza kwa ujasiri kuja mbele ya Rais Magufuli
pamoja na ugumu wa hatua hiyo. Aidha ninamuombea mafanikio kwa hatua
zinazofuata. Mungu hujibu uonevu kwa wanaomtumainia.
Katika kujadili suala hili nami sina budi kurejea tukio
kama hili mapema Januari 2, mwaka huu, Kyamyorwa mkoa wa Kagera.
Akiwa katika ziara ya kutembelea walioathirika kwa
tetemeko mkoani kwetu, Rais Magufuli alinitetea na kuniokoa mikononi mwa watesi
wangu wa muda mrefu jimboni mwangu Muleba Kusini.
Kwa sababu za kisiasa, walikuwa wananikashfu kwa kudai
nimepora ardhi ya wananchi wakati wao ndio walikuwa wakiwadanganya wananchi
wahamiaji kutoka mikoa jirani na kuwatoza fedha kwa kuwadanganya watawagawia
shamba langu la urithi kutoka kwa marehemu mume wangu.
Marehemu alimilikishwa shamba hilo kihalali miaka mingi
ya nyuma eneo likiwa pori tupu. Watu hao wanajificha nyuma ya pazia la siasa za
upinzani na huwa wanawarubuni hata maafisa wa Serikali wasiokuwa waaminifu na
wenye tamaa ya ardhi hiyo, kunisumbua.
Rais Magufuli alifika hapo na kuwakuta vijana wa
kukodishwa tayari wana mabango ya kunikashfu nimepora ardhi.
Walikuwa wanaongozwa na Diwani (tunahifadhi jina lake kwa
vile hakupatikana kuzungumzia tuhuma hiyo) wa Chadema ambaye mtaji wake wa kisiasa
ni kunikashfu, akishirikiana na wabaya wengine ngazi za juu. Awali genge hilo
kama kawaida yao walisha waandaa vijana wa kunizomea Rais Magufuli aliposimama Muleba
Mjini.
Waliamini mara baada ya kushuhudia zomeazomea, Rais
Magufuli akifika Kyamyorwa kwenye shamba langu na kukutana na mabango na kelele
dhidi yangu, ataninyang’anya shamba ili kuwafurahisha wananchi hao. Wengine
wala hawakuwa wenyeji bali walikuwa wamesombwa kutoka mbali.
Videdea vya pikipiki kutoka Kyamyorwa kuelekea Muleba
Mjini vilikuwa tayari. Mgeni rasmi kupokea maandamano hayo (jina linahifadhiwa)
tayari alikuwa Muleba akisubiri.
Lakini tofauti na mategemeo yao, Rais Magufuli msema
kweli na mpenzi wa Mungu na mtoa haki hakufurahishwa na mpango wao huo mwovu. Aliwaonya
watu wa Muleba kwamba wajitafakari ni wa aina gani. Rais alisema kabla ya
kuondoka kuelekea Kyamyorwa ambayo ni jirani na nyumbani kwake Chato.
Yaliyojiri Kyamyorwa taifa lote limeshuhudia. Rais
Magufuli aliwashushua waliokuwa wamepanga kupora ardhi yangu na katika kufanya
hivyo, kunigeuza mimi mhanga ndiye mkosaji. Rais Magufuli alieleza ukweli wa
ardhi hiyo aliyowahi kuifanyia kazi alipokuwa Waziri wa Ardhi.
Shamba limeendelezwa kwa kilimo cha mbegu bora, mifugo na
uhifadhi wa mazingira na linalipiwa kodi ya ardhi kila mwaka. Shamba lina hati
ya miaka 99.
Tukio hilo lilinipa faraja kubwa na ninalifananisha kwa
namna fulani na tukio la mjane wa jana (Februari 2) au zaidi kwa sababu Rais
Magufuli alinitetea pamoja na kwamba sikuwepo katika ziara yake hiyo.
Kwa kuwa sikujua Rais Magufuli angelisimama jimboni
kwangu Muleba Mjini, mimi mara baada ya kukamilisha ziara yake Bukoba Mjini
niliingia makubaliano na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kubaki Bukoba
Mjini kumsindikiza Katibu Mkuu Elimu.
Kwa pamoja tulimpeleka Balozi wa Uingereza, Sara Cooke
kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Rugambwa ambayo nayo imeathirika na
tetemeko ili ipewe msaada.
Mimi nilisoma Rugambwa kwa hiyo ni mdau mkubwa. Nikiwa
hapo niliweza kumueleza Balozi shule hiyo ilivyokuwa enzi zetu kama juhudi za kuhamasisha
msaada wake kwa ukarabati kama alivyotoa kwa sekondari kongwe ya Ihungo.
Kwa hiyo sikuwepo jimboni kwangu wakati wategeshi wa
siasa wananihujumu mbele ya Rais wa nchi.
Kwa hiyo kwa msaada mkubwa aliopewa mama (Shosi) na kwangu
mie na wengine ambao mambo yao labda hayapo hadharani, ninasema wanawake
tujitambue bado tuna safari ndefu.
Haijalishi wewe una elimu, cheo au nafasi gani katika
jamii. Mfumo dume unafanya kazi kukudidimiza. Ikitokea Rais aliyeshika usukani
si mtu mkweli na mcha Mungu na mtu wa haki, mwanamke utakuwa wa kwanza kulaumiwa,
kuonewa na kutolewa kafara.
Kwa mantiki hiyo wanawake ni wadau wa kwanza katika
kuhitaji kiongozi bora. Tunategemea utetezi na ulinzi wake.
Niliwahi kusema na ninarudia tena, kwa kuwa na Rais
Magufuli, Tanzania tumejaliwa kupata kiongozi siyo tu Rais, bali kiongozi
anapopewa dhana ya Urais anaitumia kama tunavyoona sasa. Kutengeneza upepo sio
kuufuata ili kufurahisha mifumo kandamizi kwa kuitolea kafara.
Nimalize makala hii na ombi. Rais Magufuli wanawake wengi
tuko nyuma yako. Tatizo la kuwanyonga vikongwe kwa kudai ardhi na haki zao katika
jamii huko vijijini bado lipo.
Ninaomba ulitupie jicho jambo hili. Kama ulivyomkabidhi
mama mlalamikaji ulinzi wa polisi uwatake wakuu wa wilaya na wakuu wa polisi wa
wilaya, kuwalinda vikongwe katika maeneo yao dhidi ya dhuluma na vitendo vya
ukatili.
0 comments:
Post a Comment