Salha Mohamed
Paul Makonda |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, ameibuka na kutaja askari zaidi ya 10 na wasanii saba wanaodaiwa
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuwataka kuripoti leo kituo kikuu
cha Polisi.
Aidha, ametoa siku saba kwa vijiwe
vinavyojihusisha na uuzaji na utumiaji wa dawa hizo kuondoka na kumtaka Kamanda
wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro na timu yake, kukosa
sifa za kuendelea kuwa askari endapo watashindwa kumaliza tatizo hilo.
Makonda alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkoa huo kukithiri watumiaji na
wauzaji wa dawa za kulevya nchini katika operesheni aliyofanya usiku wa kuamkia
jana.
“Dar es Salaam umekuwa mji wa wauzaji, wasafirishaji
na watumiaji ‘unga’ na mbaya zaidi sasa tunaanza kuhudumia mikoa mingine na
mwishowe linakuwa lango la watu kupitisha dawa za kulevya kwenda nje ya nchi.
“Wapo
askari waaminifu na waadilifu ambao wanafanya kazi kubwa kuhakikisha vita hivi vinazaa
matunda lakini wapo wasio waadilifu
ambao wamekuwa sehemu ya kuhakikisha mapambano haya hayafanikiwi,” alisema.
Alisema katika operesheni hiyo,
alijiuliza sababu ya dawa kutokwisha huku askari wakiwapo ambapo hata waendesha
pikipiki wanawajua.
“Polisi wanashindwaje kufahamu kama huyu
anafanya hiyo biashara? Sasa nimepata taarifa kwamba polisi wanashirikiana na
wafanyabiashara wa dawa za kulevya na hatimaye biashara hii kuwa ngumu
kutokomezwa,” alisema.
Aliwataka askari hao kukamatwa na
kuwekwa mahabusu kwa kushiriki na hata kuwapigia simu wauzaji kuwa wanakwenda
kuwakamata na kuwataka kuwaingizia fedha mtandaoni na anapokwenda huwakosa.
Alisema polisi wanawajua wauzaji huku
kila Jumamosi wakienda kuchukua fedha.
Makonda alisema ameamua kutimiza azma ya
Rais John Magufuli ya kumaliza tatizo hilo huku akibainisha kuwa fahari yake si
kuona idadi ya watu waliokamatwa, bali mkoa unakosa sehemu ya dawa za kulevya.
“Nilifanya utafiti mdogo nikakutana na
vijana wanaotamkwa kutumia dawa, walio kwenye vituo vya kusaidia vijana
wanaotumia dawa, nimekutana na madereva teksi wakiwamo wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kujua kwa nini tatizo la dawa za kulevya
halitokomei ndani ya mkoa wetu,” alisema.
Alisema katika utafiti huo alibaini kuwa
wanaofanya biashara hizo ni wenye uwezo mkubwa, wa kati, wasambazaji na kufikia
watumiaji.
“Mimi na ndugu zangu tumekesha leo (jana)
usiku kucha, kuona maeneo na sehemu ambazo biashara hizi wanafanya…kwa
masikitiko makubwa tumekuta biashara inafanywa hadharani tena si ngumu hata
kuifahamu na kila mtu anaifahamu.
Alisema katika biashara hiyo, wapo
wananchi wa kawaida na wageni na mbaya zaidi baadhi ya vyombo vya
Dola vikifahamu.
Makonda aliongeza: “Nimeamua kuingia
mwenyewe kwenye hivi vita kwa sababu najua siku moja Mungu ataniuliza
nilipopewa ukuu wa mkoa watoto waliangamia kwa dawa za kulevya, sitaki kufika Mbinguni
bila jibu.”
Alisema yuko tayari kupoteza ukuu wa mkoa,
kutangulia mbele za haki, lakini awe na jibu kwa Mungu wake kuwa dawa za kulevya
hazikubaliki mkoani humo.
Makonda aliongeza kuwa idadi ni kubwa
kwa wauzaji na wasambazaj, huku
akibainisha kuwapo wanaosemekana kutumia dawa hizo ambapo wakihojiwa husema na
kuwataja kuwa wanatumia wote.
“Hawa nao ni vema nikakutana nao kesho (leo),
wapo wengi …hawa wengine nimeshawatia mikononi mwa sheria nawahitaji ni vijana
wenzangu nafikiri tutaelewana vizuri,” alisema.
Alisema yapo maeneo ambayo wamepata
leseni ya biashara lakini wanafanya
biashara ya dawa za kulevya na kuonekana wazi ambapo watu wamedai kupata sehemu
hizo.
Alisema mapambano hayo si rahisi lakini
kwa kuwa walikula kiapo na Mungu kuwapa nafasi ya kuongoza, alitaka dawa za
kulevya mkoani mwake kuwa historia.
0 comments:
Post a Comment