Fidelis Butahe, Dodoma
Miaka 40 ya Chama cha Mapinduzi |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) jana kimeadhimisha miaka 40
tangu kuanzishwa kwake bila uwepo wa mwenyekiti wake, Rais John Magufuli huku
ikielezwa kuwa kiongozi mkuu huyo wa nchi atachagua siku na mahali pa
kuadhimisha sherehe hizo.
Aidha, chama hicho kimetangaza kuanza kufanya mikutano ya
ndani nchi nzima kuanzia ngazi za chini.
Mbali na kukosekana kwa Magufuli, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wa Rais,
Samia Suluhu, nao hawakuhudhuria sherehe hizo zilizofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa CCM Dodoma.
Pia, marais wastaafu, Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na
Ali Hassan Mwinyi nao hawakuhudhuria.
“Nawaletea salamu kutoka kwa mwenyekiti wetu Rais
Magufuli…, yeye atachagua siku, wapi na tarehe ya kuadhimisha miaka 40,”
alisema Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM wakati akizungumza na maelfu ya
wanachama wa chama hicho Mkoa wa Dodoma waliohudhuria sherehe hizo huku
akieleza mambo mazuri yaliyofanywa na Rais huyo wa Awamu ya Tano kwa
kuibadilisha nchi katika kila sekta, sambamba na kurejesha uwajibikaji.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo ambazo
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole alibainisha kuwa
mkoa wa Dodoma umepata bahati kutokana na viongozi wengi kuhudhuria ni Spika wa
Bunge, Job Ndugai na naibu wake, Dk Tulia Ackson.
Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu, Mizengo Pinda na John
Malecela, kada mkongwe wa chama hicho,
Job Lusinde, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Kukosekana kwa mwenyekiti huyo wa CCM kulizua maswali
miongoni mwa wanachama waliokuwepo katika ukumbi huo kabla ya ufafanuzi
kutolewa na Kinana, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole
akieleza utaratibu wa maadhimisho hayo kuwa yanafanyika kila mkoa nchini.
Katika maadhimisho ya miaka 39 sherehe hizo
zilifanyika mkoani Singida huku yale ya
38 yakifanyika mkoani Ruvuma na Mbeya yalifanyika ya 37 na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa CCM, akiwemo Rais
mstaafu Jakaya Kikwete ambaye alikabidhi kijiti cha uenyekiti kwa Dk Magufuli.
Akihusisha maadhimisho hayo kufanyika kila mkoa na kubana
matumizi, Kinana alisema maadhimisho si sherehe na kuwataka wananchi kuachana
na utaratibu wa sherehe kwa sababu wanaonufaika ni wachache.
“Wanaopata kadi za mialiko na kula vizuri ni walewale.
Maadhimisho ya siku ya uhuru pale Ikulu kuna watu wanaalikwa? Nahakika mambo
yote haya kutakuwa na malalamiko lakini ndio tunajenga uwajibikaji. Tuiunge
mkono Serikali katika kusimamia matumizi na fedha za umma,” alisema Kinana.
Awali kabla ya maelezo ya Kinana, Polepole alisema jana
haikuwa siku ya uzinduzi au kilele cha maadhimisho hayo bali wamelenga kufanya
mikutano ya ndani nchi nzima.
“Tumeona tufanye tofauti si katika uwanja wa mpira,
tumeona tukae tujadiliane tumetoka wapi, tupo wapi na tunakwenda wapi.
Maadhimisho haya mkoani hapa yanafanyika kila mkoa nchini na tunafanya hivi
mwaka mzima,” alisema Polepole.
Alisema lengo ni kujadiliana na kutoka na mwongozo kwa
mwaka 2017 ikiwa ni pamoja na kuwafanya wananchama wa chama hicho kuwafikia
wananchi.
Akitoa salamu zake kwa maelfu ya wanachama wa CCM,
Majaliwa alisema Serikali itahakikisha inatekeleza ahadi zake kwa wananchi.
“Wajibu wetu wana CCM ni kukisema chama chetu, kuisema serikali yetu na
kuhakikisha chama kinakuwa imara,” alisema.
Katika maadhimisho hayo, Mangula alieleza sababu za chama
hicho kuwa cha mapinduzi na kubainisha mambo kadhaa mazuri yaliyofanywa na
Serikali.
Kinana na siri za ushindi CCM
“Chama chetu kina sifa za kuona mbali na kujua kifanye
nini. Tunatazama nchi inakwenda wapi na watu wanafanya nini. Tukiona mbali
mazuri tunayapeleka mbele mabaya tutayasawazisha, tunafanya mageuzi kila kipindi
na kufanya tahmini kila mara, ya wazi na faragha,” alisema Kinana.
Alisema CCM kina njia mbalimbali za kupata wagombea wake
kwa kutaka kila mwanachama ashiriki na kubainisha kuwa huko ni ndio kwenda na
wakati akifafanua “Tunafanya tahmini ya namna chama kinavyokubalika. Hii
tunafanya wenyewe kwa kutumia njia zetu. Mwaka jana tumefanya tathmini ya mwaka
mmoja wa uongozi wa Rais Magufuli.”
Alisema chama hicho kikishindwa watu wanaulizana
kimeshindaje bila kujua mambo kinayoyafanya kupitia tathmini hizo na vikao
mbalimbali na kubainisha kuwa tahmini yam waka 2015 ilikuwa kabambe kutokana na
kufanyika kwa miezi 12.
“Tuliagiza kuanzia ngazi za chini za chama kutazama
wanavyokiona chama na kutuletea maoni na mapendekezo yao. Tulifanya hivi
kukiimarisha chama chetu kiendelee kuongoza na kushinda, pili kupunguza urasimu
na umangimeza ndani ya chama kama watu kukaa maofisini na kujishughulisha na
mambo yao wenyewe na kutokwenda kwa wananchi,” alisema Kinana.
Alisema lengo jingine ni kupunguza gharama za kuendesha
chama kutokana na wali kuwa na vikao vingine huku watu wakilipwa posho za mara
kwa mara.
Huku akitolea mfano wa uchaguzi wa mgombea udiwani katika
moja ya Kata nchini alisema: “Kuna mmoja alishindwa katika kura ya maoni kwa
kupata kura tisa na alikuwa Katibu wa Uenezezi ila aliyeshinda alipata kura 56,
wahusika wakaanza kuulizana watamuachaje katibu mwenezi huyo ambaye alishindwa
na mwanachama wa kawaida. Watu wa aina hii hatuwataki tena CCM.”
Alsema kazi iliyopo sasa ni kutahmini mageuzi ndani ya
chama hicho ikiwa ni pamoja na muundo wa vikao vya chama hicho kuanzia ngazi ya
shina hadi Taifa.
“Tutajadili katika Halmshauri Kuu na Kamati Kuu hivi
karibuni ila Rais Magufuli amesema kutokana na kuwa mabadiliko ni mengi
yapelekwe kwenye mkutano mkuu wa chama. Lengo la CCM ni kuwajali wananchi ndio
maana Rais Magufuli ameanza kuchukua hatua kupunguza kodi mbalimbali ili
kuwaondolea ugumu wa maisha wananchi katika biashara na shughuli zao
mbalimbali,” alisema Kinana.
Alisema chama hicho kinafanya uchaguzi wa viongozi wake
mwaka huu na kuwataka wanachama kuchagua watu makini
0 comments:
Post a Comment