Suleiman Msuya
Paul Makonda |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, jana alishindwa kutaja majina ya vigogo wa dawa za kulevya, badala yake
akamkabidhi Kamishna wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya,
Rogers Sianga majina 97 akisema ni ya vigogo na ya watoto wa viongozi.
Katika mkutano wake uliojumuisha
viongozi wa idara na taasisi za Serikali na viongozi wa dini, Makonda alisema
operesheni ya kutafuta wauzaji, wasambazaji na watumiaji inaendelea mkoani
humo, huku akibainisha kuwa na orodha ya nyumba, hoteli, klabu za muziki na
vijiwe vinavyohusisha na dawa za kulevya.
“Kuna nyumba 200, hoteli 67, klabu za
muziki zaidi ya 20, vijiwe 107 na wauza vitumbua wanaojihusisha na uuzaji wa
dawa za kulevya, vyote navifahamu,” alisema Makonda.
Alifafanua kwamba majina aliyokabidhi
kwa Kamishna Sianga ni ya watuhumiwa wa tangu Serikali ya Awamu ya Pili na yanahusisha
pia wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wenyewe, hivyo ni dhahiri yatatikisa
nchi.
Makonda alisema kundi hilo limejenga
mizizi kwa muda mrefu na kujiona kuwa ndilo lenye nguvu ya kufanya jambo lolote,
hivyo ni jukumu la wananchi wote kushirikiana na Kamishna kuhakikisha kuwa mapambano
hayo yanafanikiwa.
Alisema majina hayo ni awamu ya tatu ya
harakati anazozisimamia akishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na
wadau wengine na kuwa anaendelea na mchakato huo kwa awamu saba.
“Kamishna leo sitataja ila nakukabidhi
majina ya vigogo wa dawa za kulevya, ambao wamekuwa wakisababisha vijana wetu
kuangamia, lakini sisi tunaendelea na mchakato ambapo matarajio yetu ni hadi
awamu ya saba tunaamini kuwa tutakuwa tumekamilisha operesheni,” alisema.
Mkuu huyo alisema kampeni hiyo ya dawa
za kulevya haitaishia serikalini na kuwa itakwenda hadi katika familia huku
akisisitiza wazazi na wenyeviti wa mitaa kuendelea kutoa taarifa.
Makonda alisema hatoonewa mtu katika
mchakato huo kwa alichodai kuwa hadi wanamwita kumhoji mtu wamemchunguza vya
kutosha.
Alisema sheria ikitumika ipasavyo,
itasaidia kuondoa changamoto ambazo zinakabili nchi kukabiliana na hali hiyo,
hivyo kuwataka wananchi kushiriki kwa nguvu zote.
Makonda alisema katika mkoa wake na
Serikali hii ya awamu ya tano hataki kuona mbwembwe, kwani hazina nafasi.
Alisema wapo wauzaji ambao wanafanya
biashara hiyo bila kushiriki moja kwa moja, tofauti na kutumia simu na baada ya
kukamilisha kazi wanatupa simu husika na inafikia mahali hutumia majina ya
wanawake kusajili simu.
Makonda aliwasha taa nyekundu kwa
viongozi wa dini zote kuwa moto utawawakia bila kuacha yeyote anayehusika.
“Hili ni jiwe litahakikisha kuwa
linasaga mawe yote ili yawe unga na kumaliza adha hii ambayo inawasibu wananchi
wa Dar es Salaam, pia natoa mwito kila mmoja ashiriki kutoa taarifa,” alisema.
Kwa upande mwingine Makonda alisema
katika hoteli hasa za fukweni kuna
wateja wa kudumu ambao wanatia shaka.
Alisema pia katika uchunguzi wao
wamegundua nyumba nyingi za wanasiasa za Dar es Salaam zinahusika na biashara
hiyo na kuahidi kuwa hataachwa mtu.
Mkuu wa Mkoa alisema biashara hiyo
inagawanyika katika makundi makuu matatu; la mnufaika ambaye anapata faida,
waliopata kura kupitia walaji na wale ambao wametumia, kuona dunia ni yao na
ambao hawaelewi kinachofanyika.
“Ukitaka kuvusha watu kwenye maji
usishauriane nao kwani wanaweza kukushauri vibaya kwani wakati Rais Jakaya
Kikwete anakabidhiwa majina ya wauza dawa na kutakiwa ataje hakutaja, nimeamua
kutaja watu wanaanza kulalamika, hii vita hairudi nyuma ni endelevu ni lazima
tumalize,” alisema.
Alisema ni vema kila kiongozi na wananchi
kubadilika na kutambua kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni janga la Taifa hivyo
isitokee mtu kujaribu kukwamisha jitihada hizo.
Makonda alisema watumiaji wa dawa za
kulevya wako tayari kuua, kubaka, kuiba au kufanya jambo lolote ambalo linakwenda
kinyume na maadili ya nchi na utamaduni.
Aidha, alitoa ushauri kwa wazazi kununua
kipimo cha 5 Panel Mult Drug Test 15, 15 kupima vijana wao ili kubaini kuwa
wanatumia dawa au la.
Alisema kipimo hicho kina uwezo wa
kupima dawa za kulevya zaidi ya saba, hivyo ni vema wazazi wakavinunua ili
kuokoa jamii.
Maduka
ya fedha
Makonda pia alisema ongezeko la maduka
ya kubadilisha fedha ni moja ya vyanzo vya biashara hiyo ya dawa za kulevya.
Alisema kwa sasa Dar es Salaam ina maduka
hayo zaidi ya 250 hali ambayo inachangia utakatishaji fedha haramu kupitia
maduka hayo, hivyo kumwomba Kamishna kuangalia njia ya kutatua.
Kufukuza
watu
Alisema kutokana na hali hiyo kuonekana
kushika kasi anaweza kumfukuza mtu yeyote kwenye mkoa huo iwapo watabaini kuwa
anakwenda kinyume na maadili ya nchi.
“Sheria inaniruhusu nikiona huendani na
maadili ya mkoa wangu au ni hatari naweza kukuhamisha muda wowote na hakuna wa
kunihoji,” alitamba.
0 comments:
Post a Comment