*Ashangaa wawekezaji kushikiliwa, asema
ni hatari kwa Taifa kiuchumi
*Akaunti zake pia nazo zapekuliwa
Mwandishi Wetu
Josephat Gwajima |
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima, amemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati sakata la kutangaza
na kushikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam watu wanaotuhumiwa
kujihusisha na dawa za kulevya.
Pia alieleza kushangazwa kwake na baadhi
ya wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa nchini kuingizwa katika sakata hilo hata
kabla uchunguzi kufanyika.
Gwajima ambaye alikuwa ameshikiliwa Kituo
Kikuu cha Polisi Dar es Salaam alikokwenda baada ya kutangazwa na Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya,
alisema hana mpango wa kumshtaki mkuu huyo wa mkoa.
Askofu Gwajima alisema badala yake
anakata rufaa kwa Rais Magufuli akimtaka kufuatilia tuhuma hizo kwa undani kwa
watu wanaoendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi ili waweze kupata haki.
Akizungumza kanisani kwake Dar es Salaam
jana, Gwajima alisema alishikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam
baada ya kwenda kuitikia mwito uliotolewa na Makonda kwa ajili ya kutoa
ushirikiano kuhusu tuhuma za dawa za kulevya
Alisema baada ya kufika kituoni hapo na
kufanyiwa mahojiano alikutana na mfanyabishara na Diwani wa Mbagala Kuu, Yusuph
Manji ambaye naye alikuwa amefika kituoni hapo kwa ajili ya kuitika mwito huo
wa Makonda.
"Kwenye chumba changu tulikuwa mimi
na Yusuph Manji, huyu ana kampuni zaidi ya 23 ameajiri Watanzania zaidi ya
5,000, sasa mtu kama huyo imeshindikanaje kumuita kwa kumpelekea hati ya kuitwa
kuhojiwa, badala yake anatangazwa?"
"Imeshindikanaje mtu kama Manji
kumuita kwa kumuandikia barua ili aende ahojiwe na ikigundulika achukuliwe
hatua, kwa nini atangazwe kabla ya kuchukuliwa hatua? Ilipaswa aandikiwe barua ya wito kisha
uchunguzi ufanyike na kama akibainika ndiyo achukuliwe hatua, ila kwa sababu
mkuu wa mkoa hakuwa na nia nzuri hata kwa Manji ndiyo maana hakufanya
hivyo," alisema Gwajima.
Alisema hadi alipoachiwa katika kituo
hicho bado Manji alikuwa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi, ambapo alihoji sababu
ya Manji na wengine wanaoendelea kushikiliwa kituoni hapo kutofanyiwa uchunguzi
na ukaguzi kama aliyofanyiwa yeye ili waachiwe kama yeye au kuchukuliwa hatua
kama wakibainika kujihusisha na biashara hiyo.
"Sioni sababu ya kuendelea
kuwashikilia watu wale bila kuchukuliwa hatua. Kama mimi nilituhumiwa tena kwa
kutangazwa lakini mwishowe ikabainika hakuna ukweli, nitaamini vipi kama wale
waliobaki ndani mikononi mwa Polisi nao wanahusika?"Alihoji Gwajima.
Gwajima alisema mbali na Manji na
wafanyabishara wengine waliotajwa kuhusika na biashara hiyo, wamo pia askari wa
Polisi ambao nao wanatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo na wameendelea
kushikiliwa kwa amri ya mkuu wa mkoa.
Kutokana na hali hiyo, Gwajima alisema
ameamua kukata rufaa kwa Rais ili aweze kuwaangalia watu hao kwa jicho la tatu
na tuhuma dhidi yao ziweze kuchunguzwa na ukweli ujulikane.
"Mheshimiwa Rais ninakuomba sana,
kuna wale watu wengine ambao nilikuwa nao, ambao ni wafanyabishara na
walitangazwa kama mimi, naomba uwatazame kwa macho ya huruma ili tuhuma zao
zishughulikiwe, kuliko kuendelea kukaa kwenye giza chini mule, kwa niaba yao
ninakata rufaa kwako naomba uwahurumie.
"Kuna askari Polisi wapo ndani kwa
wiki ya pili sasa kwa amri ya Makonda, mimi naomba niwasemee leo, kama mimi
imeonekana kuwa sina makosa, vipi kuhusu wao? Nampongeza mheshimiwa Rais kwa
kuingia katika vita ya dawa za kulevya naomba atazame jambo hili, "alisisitiza
Askofu Gwajima.
Alisema kuwa alichogundua ni kuwa Rais
anahitaji msaada wake hivyo anaingia katika kazi ya kumsaidia Rais kwa maelezo
kuwa inawezekana anapata taarifa zisizo za ukweli.
Gwajima alisema kuwa leo amepanga kwenda
Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuwaona watuhumiwa wengine ambao wanaendelea
kushikiliwa.
Aeleza alivyokaguliwa
Katika hatua nyingine, Gwajima alisimulia
waumini wa kanisa lake namna shughuli ya ukaguzi dhidi yake ilivyoendeshwa na
Jeshi la Polisi, huku akidai amechiwa baada ya kubainika tuhuma dhidi yake
hazikuwa na ukweli.
Alisema baada ya kuhojiwa alielezwa
anatakiwa kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ili
kubaini kama anajihusisha na utumiaji wa
dawa za kulevya ama la, ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake
ambapo alieleza kuwa licha ya kufanyiwa yote hayo Polisi walifikia pia hatua ya
kukagua akaunti zake za fedha.
"Kwa sababu mimi tangu kuzaliwa
sijawahi kuonja mambo hayo, lakini walivyopima wakakuta hamna chochote na
wakanipa fomu kuonesha hawajakuta kitu.
"Niliwaambia kwangu mkikuta hata
kipisi cha sigara andikeni dawa za kulevya, tulifika kwangu nyumba yangu ina
ghorofa tatu wakakagua zote na hawakukuta kitu walichotaka," alisema
Aliongeza kuwa,"wakaona haitoshi,
wakahamia kwenye akaunti zangu za benki na mimi nikawaruhusu waendelee
walipofanya uchunguzi wao wakabaini hakuna kitu cha kuweza kunikamatia,
hawakupata kitu wakaamua kuniachia,".
Gwajima alisema hana mpango wa kumshtaki
Makonda ama kumfungulia kesi bali anajua cha kumfanya.
Dk Slaa aibuka
Aidha, Gwajima aliwaeleza waumini wa
kanisa hilo kuwa wakati akiwa mikononi mwa Polisi, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk.Willibrod Slaa alimtumia ujumbe wa kumpa pole na kumweleza kuwa
hakubaliani na tuhuma hizo na atakuwa tayari kutoa ushirikiano wa ushahidi
kumhusu.
0 comments:
Post a Comment