Fidelis Butahe, Dodoma
MKUTANO wa Sita wa Bunge la 11 uliomalizika Ijumaa
iliyopita mjini hapa, umeandika historia nyingine kutokana na kuwepo kwa mambo
makuu matano yaliyolipa Bunge hilo sura tofauti na mikutano mingine iliyopita.
Kwa pamoja wabunge wote bila kujali itikadi zao za vyama
vya siasa walisimamia walichokiamini hivyo kukipa chombo hicho hadhi yake.
Mambo hayo ni pamoja na kupinga wakuu wa mikoa na wilaya
kuingilia haki na madaraka ya Bunge, wabunge kukamatwa bila utaratibu, kasoro
katika kutaja watu wanaotakiwa kuhojiwa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za
kulevya, kuhoji utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 na kusuasua kwa
utekelezaji wa sera ya Tanzania kuhusu viwanda.
Tofauti na mikutano iliyopita, mkutano huo ulishuhudia
wabunge wakiungana katika hoja hizo bila kujali itikadi zao, jambo ambalo
liliwaweka katika wakati mgumu baadhi ya mawaziri huku Spika Job Ndugai
akihitimisha kwa kuonya wateule wa Rais wanaojisahau kwa kutoa lugha zisizoeleweka.
Madaraka ya Bunge
Kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
kuita mkutano wa waandishi wa habari na kuwataja watu kadhaa akiwataka kufika
Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, ndicho kilichoibua hoja ya kuingiliwa na
kupuuzwa kwa madaraka ya Bunge.
Mjadala kuhusu suala hilo uliibuliwa na Mbunge wa Ukonga,
Mwita Waitara (Chadema) kupitia kanuni ya 52.
Katika hoja yake, Waitara alisema Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,
Alexander Mnyeti walitoa matamshi yanayoingilia haki na madaraka ya Bunge.
Waitara alisema Makonda wakati akizungumza na wanahabari,
alisema wabunge huwa wanakwenda bungeni kusinzia, kauli ambayo inakiuka Sheria
ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Kuhusu Mnyeti, alisema mkanda wa video yake umesambaa
katika mtandao wa facebook ukimnukuu akisema; “huu ni upuuzi mtupu, wabunge
hawa hawajielewi nawashauri mfanye kazi zenu.”
Hoja ya Waitara ambayo siku moja nyuma iliibuliwa na Mbunge
wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM) na Bunge kuazimia Makonda kuandika maelezo ya
kujieleza kwa kauli yake hiyo ambapo iliungwa mkono na wabunge wote na
kutaka hatua zichukuliwe ili kurejesha hadhi ya mhimili huo.
Baada ya Waitara kutoa maelezo yake, wabunge mbalimbali
walichangia na kubainisha kuwa Serikali haiwezi kujengwa na viongozi wenye
kiburi.
“Unapotaka kulitoa pepo mheshimiwa mwenyekiti
halibembelezwi. Unataka kuyapunga majini huwezi kubembeleza. Lazima ukazane
kulipunga jini litoke. Hatuwezi kutoa pepo kwa lugha nyepesi nyepesi (akipunguza
sauti) pepo toka, haiwezekani. Kama ni pepo tulikemee litoke,” alisema John
Kidutu, Mbunge wa Ulyankulu (CCM).
Hoja hiyo ilihitimishwa kwa Bunge kupitisha maazimio
manne bila kusikia sauti ya “siyooo” kutoka miongoni mwa wabunge, likiwemo la
kuwaita wateule hao wawili wa Rais kuhojiwa na mhimili huo kwa matamshi yao.
Wabunge kukamatwa
Hoja ya wabunge kukamatwa bila Bunge kuwa na taarifa
lilikuwa ni moja ya maazimio hayo manne yaliyopitishwa kwenye mkutano huo, huku
Spika wa Bunge, Ndugai wakati akiahirisha Bunge aliagiza mtu anayemtaka mbunge
ni lazima atoe taarifa kwake.
Ndugai alionya kuwa,“wakati mwingine akikosekana mbunge
mmoja inawezekana mambo kwenye kamati yasitekelezwe. Kwa hiyo kama kuna ofisa yeyote
anamhitaji mbunge, lazima aniambie. Hatuwezi kwenda hivyo. Kwa hakika kwenda
hivyo kibabebabe kutaivuruga nchi.”
Kutajwa majina
Sakata la kutangaza hadharani majina ya watu wanaotakiwa
kuhojiwa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya ililiwaamsha wabunge na
kutoa kauli zilizoonesha kutokubaliana na utaratibu unaotumika katika vita dhidi
ya dawa hizo haramu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama, Balozi Adadi Rajabu wakati akihitimisha michango ya wabunge kuhusu
taarifa ya kamati hiyo alisema:
“Upelelezi wa kesi za jinai hauwezi kufanywa kwa kutaja
majina ya watu hadharani. Kufanya hivyo ni kupoteza ushahidi mahakamani.”
Utekelezaji bajeti
Katika mkutano huo kamati mbalimbali za Bunge
ziliwasilisha taarifa za kuanzia Januari 2016 hadi Januari mwaka huu, huku
kukiwa na upungufu mkubwa katika utekelezaji wa bajeti za maendeleo katika
wizara mbalimbali.
Katika uchambuzi uliofanywa na gazeti hili hakuna wizara
hata moja iliyopata asilimia 45 ya bajeti ya fedha za maendeleo, jambo ambalo
wabunge walihoji na kueleza wasiwasi wao kuhusu utekelezaji huo.
Mathalan, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji hadi kufikia
Januari mwaka huu imepatiwa sh. bilioni 7.6 ya fedha za maendeleo sawa na
asilimia 18.6.
Licha ya fedha hizo kutotolewa, Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk. Philip Mpango alilieleza JAMBO LEO kuwa Serikali inatekeleza
bajeti yake kulingana na inavyokusanya na kusisitiza kuwa miradi mingine ya
maendeleo ni endelevu.
“Utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa awamu.
Hivyo ndivyo ilivyo, mfano ujenzi wa darasa unakuwaje? ni suala la awamu tu,”
alisema Dk. Mpango.
Tanzania ya Viwanda
Suala la Tanzania kuwa nchi ya viwanda nalo lilitikisa
Bunge huku wabunge wakionesha wasiwasi hao kama sera hiyo itatekelezeka.
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alisema Serikali
haiwezi kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama haijajua sababu zilizoua
viwanda vilivyokuwapo.
Alisema badala ya Serikali kusisitiza uanzishwaji wa
viwanda vipya, ingeimarisha viwanda vilivyopo ili vizalishe kwa mafanikio zaidi
kwa sababu baadhi havina malighafi za kutosha.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage
naye alijikuta katika wakati mgumu baada ya Kamati ya Bunge ya Viwanda,
Biashara na Mazingira kusema haina taarifa yoyote ya kuanzishwa kwa viwanda
1,169 nchini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Dalaly Kafumu alisema,
“Viwanda ambavyo vimesemwa na Ulega ni 67, Waziri anasema ana viwanda 1,169.
Mimi nataka niseme hili, kamati yangu haina taarifa kabisa,”alisema Dk Kafumu.
“Tafsiri yetu kama kamati ni kuwa waziri hushirikiani
na sisi vizuri kwa sababu tungekuwa tuna habari hata kufunguliwa kwa kiwanda
cha Mkuranga. Tungejua angeweza kwenda mwenyekiti wa kamati au hata mjumbe
mmoja tu. Habari tungekuwa nazo.”
0 comments:
Post a Comment