Stella Kessy
BARAZA la Viongozi wa Dini la Kupambana
na Dawa za Kulevya Tanzania lililo chini ya Tume ya Kupambana na Dawa za
Kulevya, limeomba mamlaka husika kumuongezea ulinzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda, kwa kuthubutu kutaja watuhumiwa wa dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Salum ambaye ni Mwenyekiti wa kamati
hiyo, alisema ujasiri alioonesha Makonda kwa kujitoa mhanga kwa ajili ya Taifa
na watu, umeonesha uthubutu unaohitaji kuungwa mkono.
"Sisi Baraza tunapinga vita na
kulaani hatua yoyote ya kushiriki katika biashara au utumiaji wa dawa za
kulevya, kwa kuwa matumizi ya dawa hizo yamekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo
katika nchi yetu na yanapoteza nguvu kazi ya Taifa huku waathirika wakubwa wa
matumizi ya dawa hizo wakiwa vijana,"alisema.
Alifafanua kuwa endapo kiongozi wa dini
atabainika kushiriki katika matumizi ya dawa za kulevya, Baraza litamwita na
kumuonya ili ajiepushe na dawa zilizoangamiza vijana wengi hapa nchini.
Shekhe Salum alisema kutokana na ugumu
wa kazi hiyo, wanaendelea kumwombea Mungu ili Makonda afanyekazi hiyo kwa
ukamilifu itakayosaidia kukomboa nguvu kazi ya Taifa ambayo waliowengi ni waathirika
wa matatizo ya dawa za kulevya.
"Kutokana na ugumu wa kazi hiyo
tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu ili ampe ulinzi na kinga, pia azidi kumpa moyo
wa uajsiri wa kupambana na maovu yote yanayoharibu sifa ya Taifa letu na vijana
wetu," alisema.
Aliwaomba wananchi wote kumuunga mkono
na kumpa ushirikiano wa kutosha Makonda kwa uthubutu ambao ameonesha ili
kujenga Taifa imara la wachapakazi.
0 comments:
Post a Comment