Celina Mathew
MGOGORO wa CUF umeendelea kupata sura mpya,
baada ya upande wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, kutoa kauli ikionesha hofu
ya usalama wao na ofisi za chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye
ofisi hizo jana, Mkurugenzi wa Ulinzi
na Usalama wa CUF, Masoud Mhina alidai kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius
Mtatiro na wenzake, wamepanga kuvamia ofisi za chama hicho.
Mhina alidai tayari walinzi wa chama
wamejipanga kukabiliana na kikundi chochote chenye dhamira ya kuhujumu chama
hicho.
“Tuna taarifa kuwa kuna vijana wanaandaliwa
kuja kuvamia ofisi kuu za chama Buguruni kwa ajili ya kufanya vurugu, nadhani wanatufahamu
vizuri, tukianza huwa hatukamatiki na tutahakikisha chama kinabaki salama,”
alidai.
Mhina alidai wanawafahamu viongozi
waliopanga hujuma hizo na tayari wamewasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu
vitisho na vitendo vya udhalimu vinavyokusudiwa kufanywa na wasaliti wa chama hicho,
dhidi ya viongozi wa chama upande wa Bara.
Alidai kwa sasa hawawezi kuweka wazi
majina ya viongozi hao kwa kuwa wanajijua na vikao wanavyofanya kila kukicha
ila ipo siku watawataja ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria na
kikatiba.
“Tutawashughulikia kisheria na kikatiba
wanaotaka kuhujumu chama kokote waliko tutawatafuta hadi maeneo ambayo wanafanyia
mikutano na kuwakamata, maana CUF hatuna mgogoro, ulishamalizwa na Msajili wa
Vyama vya Siasa,” alidai.
Mhina alitoa onyo kwa wanaojiita
viongozi wa CUF wanaozungumzia vichochoroni na kuwataka kama ni halali, waache
na badala yake waende ofisi za chama hicho ili wamweleze Profesa Lipumba
walipewa uongozi na nani.
“Tumewavumilia sana kiasi cha kutosha,
sasa dawa yao ipo jikoni mmoja mmoja baada ya mwingine tutawajibika nao, hivyo
nachukua nafasi hii kutoa onyo kwao kama ni viongozi, bora waje ofisini si
kuzungumzia vichochoroni,” alisema.
Awali akizungumzia kazi za Kamati ya Ulinzi
na Usalama wa Chama, Mhina alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF ibara ya 88 (2)
(a), Katibu atakuwa Mtendaji Mkuu wa Kamati na Ibara ya 87 (1) imeeleza kuwa
wajibu wa Kamati hiyo ni kuhakikisha usalama wa chama unakuwapo nchini.
Alitumia nafasi hiyo kumsihi Katibu Mkuu
aache vikao vya kuhujumu chama, kwa kuwa havina tija kwake zaidi ya kujenga
uhasama dhidi ya wanachama na viongozi hao Bara na Zanzibar.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mtatiro
alihoji kuwa tangu lini Mwenyekiti wa Chama akachaguliwa na Msajili na kuongeza
kuwa Buguruni pamejaa wahuni wanaomlinda Lipumba, hivyo hawawezi kufika eneo
hilo.
“Hatuwezi kufanya upuuzi kama huo wa
kwenda pale na hakuna anayetaka kuvamia, kwa kuwa hakuna anayetaka kukaa kwenye
ofisi ile kimabavu kama Lipumba, tena kwa msaada wa wahuni na Polisi, sasa
tunakwenda kuhujumu nini na ili iweje?”Alihoji.
Alihoji wanaojiita wakurugenzi,
wameteuliwa na nani wakati hawamtambui Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF.
Kwa mujibu wa Mtatiro, ili mtu awe Mkurugenzi
lazima ateuliwe na Mwenyekiti halali wa chama anayetambuliwa na vikao vya
kitaifa hivyo haelewi waliteuliwa na nani.
0 comments:
Post a Comment